Aug 03, 2020 07:51 UTC
  • Boko Haram yaua watu 15  kaskazini mwa Cameroon

Wanamgambao wanaoshukiwa kuwa wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram wameua watu 15 na kuwajeruhi wengine 5 katika shambulio la guruneti walilofanya katika kambi ya raia wasio na makazi jana Jumapili huko kaskazini mwa Cameroon.

Magaidi hao wa Boko Haram walilirushia guruneti kundi la watu waliokuwa wamelala ndani ya kambi hiyo katika kijiji cha Nguetchewe. Hayo yameelezwa na Meya wa wilaya ya Mozogo, Medjeweh Boukar. Kambi hiyo iliyoshambuliwa na Boko Haram inawahifadhi watu wapatao 800.

Magaidi wa kundi la kitakfiri la Boko Haram 

Kijiji hicho kilichokumbwa na shambulio la magaidi wa Boko Haram kinapatikana katika wilaya ya Mozogo karibu na mpaka wa Nigeria kaskazini mwa Cameroon.  

Meya wa wilaya ya Bozogo amethibitisha kuuliwa watu 15 ndani ya kambi hiyo. Aidha alisema majeruhi walipelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu. Ameongeza kuwa, wafanya shambulio hilo walifika kambini hapo wakiwa na mwanamke ambaye alikuwa amebeba guruneti na kuingia hadi kambini. Wanawake na watoto ni  miongoni mwa watu waliouawa. Wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wa kundi la Boko Haram katika miezi kadhaa ya karibuni wamefanya mashambulizi na hujuma mbalimbali zipatazo ishirini huko kaskazini mwa Cameroon.

 

Tags