Misri yataka vita dhidi ya magaidi nchini Syria viongezewe kasi
(last modified Mon, 05 Oct 2020 08:10:29 GMT )
Oct 05, 2020 08:10 UTC
  • Misri yataka vita dhidi ya magaidi nchini Syria viongezewe kasi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amefanya mazungumzo na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa na kutilia mkazo udharura wa kupambana vilivyo na kikamilifu na magenge ya kigaidi nchini Syria.

Hayo yameripotiwa na mtandao wa habari wa al Yaum al Sabi'i na kuongeza kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Shoukry, amefanya mazungumzo na Geir Pedersen, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria ambaye naye ametilia mkazo nafasi muhimu ya Misri katika juhudi za kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa Syria.

Ahmad Hafidh, Msemaji rasmi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri kwa upande wake amesema, Pedersen na Shoukry wamejadiliana pia njia za kimsingi na amilifu za kuweza kuutatua kikamilifu mgogoro wa Syria.

Kilichotiliwa mkazo zaidi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri katika mazungumzo hayo ni kukomeshwa mapigano na udharura wa kupambana vilivyo na magenge ya kigaidi na waungaji mkono wao pamoja na kukabiliana kikamilifu na misimamo mikali.

Magaidi wa ISIS

 

Pande mbili za Misri na Umoja wa Mataifa aidha zimeelezea matumaini yao kwamba mchakato wa kisiasa utapiga hatua kubwa zaidi katika hatua ya baadaye na kutashuhudiwa mabadiliko chanya katika kamati ya Katiba mpya na kuanza utekelezaji kamili wa azimio nambari 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mgogoro wa Syria ulianzishwa mwaka 2011 baada ya maadui wa taifa hilo la Kiarabu kutumia fedha nyingi kumimina nchini humo magenge ya kigaidi kutoka kila kona ya dunia kwa tamaa ya kuipindua serikali inayotawala kikatiba nchini humo.

Viranja wakuu wa uadui huo dhidi ya taifa la Syria zilikuwa ni Saudi Arabia, Marekani, utawala wa Kizayuni na vibaraka wao. Hata hivyo njama zote zimefeli kutokana na uungaji mkono mkubwa wa wananchi wa Syria kwa serikali yao, ukakamavu wa jeshi, ushauri wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na msaada wa Russia. Genge la kigaidi la Daesh ISIS na magenge mengine yote yamesambaratishwa Syria na kubakia baadhi tu.

Tags