Upinzani: Watu 90 wameuawa katika ghasia za kabla ya uchaguzi Guinea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63986-upinzani_watu_90_wameuawa_katika_ghasia_za_kabla_ya_uchaguzi_guinea
Kundi moja la kiraia limesema makumi ya watu wameuawa nchini Guinea katika maandamano ya machafuko ya kabla ya uchaguzi wa rais utakaofanyika Oktoba 18 mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 13, 2020 03:42 UTC
  • Upinzani: Watu 90 wameuawa katika ghasia za kabla ya uchaguzi Guinea

Kundi moja la kiraia limesema makumi ya watu wameuawa nchini Guinea katika maandamano ya machafuko ya kabla ya uchaguzi wa rais utakaofanyika Oktoba 18 mwaka huu.

Kundi hilo la National Front for the Defence of the Constitution (FNDC) ambalo linakosoa vikali hatua ya Rais wa nchi hiyo Alpha Conde mwenye umri wa miaka 82 ya kuwania urais kwa muhula wa tatu wenye utata wa kisheria limesema watu 92 wameuawa katika ghasia hizo.

Katika taarifa jana Jumatatu, kundi hilo limesema miongoni mwa waliouawa, ni raia 45 waliopigwa risasi na maafisa usalama kwa kushiriki maandamano ya kupinga hatua ya Conde ya kuwania urais, yaliyoanza katikakati ya mwezi Oktoba mwaka uliopita. 

Mchafuko hayo yalishtadi mwezi Machi mwaka huu, baada ya kufanyika kura ya maoni iliyomfungulia mlango Conde kugombea muhula huo tata wa urais. 

Hata hivyo Waziri wa Usalama wa Guinea, Albert Damantang Camara amepuuzilia mbali madai na takwimu hizo za FNDC akisisitiza kuwa ni za kisiasa na hazina msingi wowote, na kwamba zimetolewa kwa maslahi ya upinzani.

Polisi ya Guinea ikikabiliana na maaandamano ya wapinzani mjini Conackry

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya Umoja wa Mataifa kutahadharisha kuhusu kauli za chuki za kikabila zinazozidi kutolewa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi huo na kuonya kuwa hali ya mambo nchini humo ni "hatarishi mno" na inaweza kusababisha kutokea machafuko.

Siku chache zilizopita, shirika la kuteteta haki za binadamu la Amnesty International lilieleza katika ripoti kuwa, watu wasiopungua 50 waliuliwa katika ukandamizaji uliofanywa mwezi Julai na kuikosoa serikali kwa kushindwa kuviwajibisha vikosi vya usalama.