Maelfu ya wapinzani waandamana Algeria kuunga mkono harakati ya Hirak
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i66946-maelfu_ya_wapinzani_waandamana_algeria_kuunga_mkono_harakati_ya_hirak
Maelfu ya watu waliandamana jana katika mji wa Kherrata nchini Algeria kuunga mkono Harakati ya Hirak ambayo ilimuondoa madarakani rais mkongwe Abduaziz Bouteflika mwaka 2019. Maandamano hayo yalisitishwa baada ya kuanza maambukizi ya COVID-19 mwaka jana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 17, 2021 04:28 UTC
  • Maelfu ya wapinzani waandamana Algeria kuunga mkono harakati ya Hirak

Maelfu ya watu waliandamana jana katika mji wa Kherrata nchini Algeria kuunga mkono Harakati ya Hirak ambayo ilimuondoa madarakani rais mkongwe Abduaziz Bouteflika mwaka 2019. Maandamano hayo yalisitishwa baada ya kuanza maambukizi ya COVID-19 mwaka jana.

Zaidi ya waandamanaji 5,000 wamemiinika mitaani wakiwa wamebeba bendera za Algeria huku wakitoa nara kama vile: "Tunataka serikali ya kiraia na si serikali ya kijeshi", na 'Genge lazima liondoke."

Maandamano hayo ya Jumanne yalifanyika kuadhimisha mwaka wa pili wa kuanza maadamano ya mwaka 2019, ambayo yalianzia Kherrata, mashariki mwa mji mkuu Algiers, kabla ya kuenea kote katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria

Harakati ya Hirak inasisitiza kuwa mfumo wote wa kisiasa uliotawala Algeria kwa miongo kadhaa unapaswa kuondoka. Hata baada ya Abdelazizi Boutelika kuondolewa madarakani Aprili 2019, maelfu ya Waalgeria waliandamana wakisisitiza kuwa vibaraka wake bado walikuwa madarakani. Mrithi wa Bouteflika, Abdelmadjid Tebboune, alichaguliwa Disemba 2019 katika uchaguzi ambao Harakati ya Hirak iliutaja kuwa ni wa kimaonyesho tu.

Maandamano ya kila wiki ya Harakti ya Hirak yalisitishwa baada ya kuenea maambukizi ya COVID-19 ambayo yalipelekea shughuli nyingi za umma kusitishwa Algeria.

Ingawa Harakati ya Hirak haijatangaza viongozi wake, lakini waungaji mkono wake wamekuwa wakifanya mijadala katika mitandao ya kijamii kwa lengo la kuanza tena maandamano ili kudai mabadiliko.