Manung'uniko baada ya Equatorial Guinea kusema itahamishia ubalozi wake Quds
(last modified Sat, 20 Feb 2021 12:42:01 GMT )
Feb 20, 2021 12:42 UTC
  • Manung'uniko baada ya Equatorial Guinea kusema itahamishia ubalozi wake Quds

Hatua ya mtawala wa muda mrefu wa Equatorial Guinea kusema kuwa nchi hiyo itauhamishia ubalozi wake mjini Quds Tukufu unaokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel kutoka Tel Aviv imekosolewa vikali ndani ya nje ya nchi.

Rais Teodoro Obiang Nguema wa Equatorial Guinea alitoa tangazo hilo jana Ijumaa katika mazungumzo yake ya simu na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, akidai kuwa nchi hiyo itakuwa ya pili ya Kiafrika baada ya Malawi, kuchukua hatua hiyo.

Tangazo hilo limelalamikiwa vikali na wanaharakati wa kisiasa ndani na nje ya nchi. Ras Mubarak, mbunge wa Ghana amezungumzia hatua hiyo na kubainisha kuwa, "Equatorial Guinea ni nchi yenye utawala wa kidikteta na isiyo na demokrasia. Hii ni nchi isiyoheshimu haki za binadamu wala utawala wa sheria."

Amesema utawala huo unajaribu kuunyooshea mkono utawala wenye mienendo kama yake, nao ni utawala wa mfumo wa kibaguzi wa Israel.

Rais Nguema

Rais Obiang Nguema mwenye umri wa miaka karibu 80 amekuwa madarakani nchini humo tangu mwaka 1979, na anahesabiwa kuwa rais aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi duniani.

Novemba mwaka jana, Malawi ilitangaza kuwa ina mpango wa kufungua ubalozi katika mji mtukufu wa Quds huko Palestina unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

Disemba mwaka 2017, aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump alichukua uamuzi wa upande mmoja wa kuutambua mji mtakatifu wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, na kutangaza kuhamishia ubalozi wa Washington  mjini Beitul-Muqaddas. Licha ya propaganda kubwa ya mpango huo, hadi sasa ni nchi chache ambazo zimefuata mkumbo huo.