Wananchi wa Congo Brazaville wapiga kura, Nguesso atazamiwa kushinda
Wananchi wa Jamhuri ya Congo Brazaville wanaelekea katika masanduku ya kupigia kura leo Jumapili kushiriki uchaguzi wa rais ambao umesusiwa na chama kikuu cha upinzani nchini humo.
Rais Denis Sassou Nguesso ambaye ameiongoza nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta kwa miaka 36 anatazamiwa kuibuka mshindi kwa muhula wa nne katika uchaguzi huo. Watu milioni 2.5 kati ya milioni tano inayounda jamii ya watu wote wa nchi hiyo wamesajiliwa kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa leo.
Sassou Nguesso mwenye umri wa miaka 77 na anayewania muhula mwingine wa miaka mitano atachuana na wagombea sita wa upinzani katika uchaguzi huu.
Mwishoni mwa Januari mwaka huu, chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Pan-African Union for Social Democracy (UPADS) kilitangaza kuwa hakitakuwa na mgombea wa urais katika uchaguzi wa leo Jumapili, kikidai kuwa mazingira ya sasa nchini humo si mazuri kwa ajili ya zoezi hilo la kidemokrasia. Kilisema uchaguzi huu utasababisha mgawanyiko zaidi nchini humo.
Guy Brice Parfait Kolelas, kinara wa chama cha Union of Humanists Democrats mwenye umri wa miaka 61 ndiye mgombea anayetazamiwa kumpa ushindani mkubwa Rais Nguesso katika uchaguzi wa leo. Hata hivyo familia yake imearifu kuwa mwanasiasa huyo wa upinzani amelazwa hospitalini baada ya kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19.
Ikumbukwe kuwa, mwaka 2016, machafuko ya uchaguzi yalishuhudiwa nchini humo baada ya Denis Sassou Nguesso kushinda tena kiti cha rais wa nchi hiyo kwa kupata asilimia 60 ya kura zilizopigwa.