Mamia wamepoteza maisha, zaidi ya milioni 1 wahama makazi yao kutokana na mafuriko huko Niger
(last modified Wed, 09 Oct 2024 13:58:24 GMT )
Oct 09, 2024 13:58 UTC
  • Mamia wamepoteza maisha, zaidi ya milioni 1 wahama makazi yao kutokana na mafuriko huko Niger

Mvua kubwa iliyonyesha nchini Niger imesababisha vifo vya watu 339 na kuwalazimisha wengine zaidi ya milioni 1.1 kuhama makazi yao tangu mwezi Juni mwaka huu hadi sasa.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Niger mwezi uliopita alitangaza kuwa takriban watu 273 walipoteza maisha na zaidi ya 700,000 waliathirika wakati hali mbaya ya hewa ilipoikumba nchi hiyo ya eneo la  Sahel barani Afrika. 

Ameongeza kuwa hadi kufikia Septemba 23, mafuriko yalikuwa yameathiri zaidi ya watu milioni 1.1, na kusababisha vifo vya watu 339, na wengine 383 kujeruhiwa.

Maeneo mengi ya Niger yameathiriwa na mafuriko ukiwemo mji mkuu, Niamey, ambapo watu tisa wameripotiwa kuaga dunia. 

Mafuriko hayo pia yamesababisha "hasara kubwa ya mali, mifugo na mazao ya chakula.

Msikiti wa kihistoria katika mji wa pili wa ukubwa wa Niger, Zinder, uliojengwa katikati ya karne ya 19, pia umeharibiwa.

Baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika yamerekodi mvua kubwa, zaidi ya asilimia 200 ikinganishwa na miaka iliyopita.

Kutokana na uharibifu wa shule na idadi kubwa ya familia zilizopoteza makazi, serikali imeahirisha kuanza kwa mwaka wa masomo hadi mwisho wa Oktoba.