Jenerali Tchiani kuiongoza Niger kwa mpito wa miaka 5
Kiongozi wa kijeshi wa Niger ameapishwa rasmi kuwa rais wa nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika kwa kipindi cha mpito cha miaka mitano.
Jenerali Tchiani jana Jumatano alichukua rasmi wadhifa wa urais chini ya Hati mpya ambayo inachukua nafasi ya Katiba ya nchi hiyo ya Kiafrika. Kadhalika amepandishwa ngazi hadi cheo cha juu zaidi cha kijeshi cha jenerali; ambapo pia amesaini dikrii ya kuamuru vyama vyote vya kisiasa vivunjwe.
Wakati wa hafla ya kula kiapo katika mji mkuu, Niamey, Jenerali Tchiani alisema kuhusu cheo chake kipya cha kijeshi kuwa, "Ninapokea nishani hii kwa unyenyekevu mkubwa... nitajitahidi kutekeleza majukumu yangu kwa mujibu wa imani walionayo (Waniger) kwangu."
Mpito wa kuelekea kwenye utawala wa kidemokrasia unaenda sambamba na mapendekezo ambayo tume maalumu iliyobuniwa ilitoa kufuatia midahalo ya kitaifa. Kwa mujibu wa katiba hiyo mpya, kipindi hiki cha mpito cha miaka mitano "kinaweza kubadilika" kulingana na hali ya usalama wa nchi.
Tofauti na watawala wa kijeshi nchini Mali na Burkina Faso, maafisa wa Niger walisitisha operesheni ya kijeshi ya Ufaransa ya Barkhane na kuvitimua vikosi vya Ufaransa pamoja na vikosi vingine vya Ulaya nchini humo, na kugeukia Russia kuwasaidia kupambana na ugaidi katika eneo la Sahel.
Viongozi wa Niger wanasisitiza kuwa, kufuatia mapinduzi ya Julai 2023, ambayo yalimuondoa madarakani Rais Mohammad Bazoum na kumuingiza uongozini Tchiani, Niger ilipata uhuru na 'kujinyakulia' tena mamlaka yake ya kujitawala.