Wanafunzi 50 kati ya 300 waliotekwa Nigeria wafanikiwa kutoroka
-
Wanafunzi 50 kati ya 300 waliotekwa Nigeria wafanikiwa kutoroka
Wanafunzi 50 kati ya 300 waliotekwa nyara na watu waliojihami kwa silaha kwenye jimbo la katikati mwa Nigeria la Niger, wamefanikiwa kuwatoroka watekaji wao.
Kulingana na Chama cha Kikristo cha Nigeria, watoto hao waliotoroka kati ya Ijumaa na Jumamosi tayari wameungana na wazazi wao.
Jumla ya wanafunzi 303 na walimu 12 wametekwa nyara na watu wenye silaha wasiojulikana likiwa ni tukio la pili kubwa kutokea ndani ya wiki moja, huku hofu za usalama zikiongezeka katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika.
Taarifa ambayo katibu wa serikali ya Jimbo la Niger aliitoa siku ya Ijumaa ilisema, mamlaka husika, awali zilipokea indhari ya kiintelijensia ya kuongezeka matishio ya kiusalama katika eneo hilo.
Wachambuzi wa masuala ya usalama na wakazi wa eneo hilo wamefananisha utekaji huo wa Jimbo la Niger na ule maarufu wa Chibok mwaka 2014, wakati wasichana karibu 300 walipotekwa nyara na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika Jimbo la Borno.
Wakati huo huo, Rais wa Nigeria Bola Tinubu amewapatia majukumu ya kipolisi walinzi wa kundi la "vigogo" na kuamuru maelfu ya maafisa wapya kuajiriwa kutokana na mgogoro wa kiusalama, hii ikiwa ni kulingana na ofisi yake.
Rais Tinubu anakabiliwa na mashinikizo baada ya karibu watu 400, zaidi ya 300 kati yao wakiwa wanafunzi, kutekwa nyara katika moja ya wimbi kubwa zaidi la utekaji nyara nchini humo katika siku za hivi karibuni.