Larijani: Ushirikiano wa Iran na Pakistan unachangia amani ya kikanda
Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran (SNSC), amesema ushirikiano kati ya Tehran na Islamabad katika nyanja mbalimbali unaimarisha amani na utulivu wa kieneo, na kuangazia nafasi muhimu ya Pakistan katika uwanja huo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili mjini Islamabad leo Jumanne asubuhi, Ali Larijani amesema, "Pakistan ni nchi muhimu katika eneo na ina nafasi maalum katika kuathiri usalama wake."
Akiashiria uhusiano wa "kina na wa kihistoria" uliopo kati ya nchi hizi mbili ameongeza kuwa, "leo, kwa kuzingatia matukio ya eneo, ushirikiano kati ya Iran na Pakistan katika nyanja mbalimbali unaweza kuchangia amani na utulivu wa eneo."
Larijani amepanga kukutana na maafisa wa ngazi za juu wa kisiasa na kijeshi wa Pakistan katika safari yake ya siku mbili inayokusudia kuimarisha ushirikiano wa pande mbili na kuendeleza makubaliano ya pamoja, hasa kuhusu usalama wa kikanda, usimamizi wa mpaka, kupambana na ugaidi, biashara na masuala mengine muhimu yanayohusu ulimwengu wa Kiislamu.
Akizungumzia uungaji mkono wa Pakistan kwa Iran wakati wa hujuma za Marekani na Israel mwezi Juni, ameongeza kuwa: "Wairani hawatasahau kwamba wakati wa vita vya siku 12 vya utawala wa Kizayuni na Marekani dhidi ya Iran, taifa la Pakistan lilisimama upande wa taifa la Iran."