Makamanda 11 wa ugaidi wauawa katika operesheni za jeshi la Nigeria
(last modified Thu, 08 May 2025 07:04:52 GMT )
May 08, 2025 07:04 UTC
  • Makamanda 11 wa ugaidi wauawa katika operesheni za jeshi la Nigeria

Takriban vinara 11 wa magenge ya kigaidi nchini Nigeria wameuawa na vikosi vya serikali katika operesheni za kupambana na ugaidi katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika.

Waziri wa Ulinzi wa Nigeria, Mohammed Badaru amewaambia waandishi wa habari katika mji mkuu Abuja kwamba, mmoja wa viongozi wa kigaidi "wanaotafutwa sana" katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, anayetambulika kwa jina la Bello Turji, amekuwa akitoroka kutokana na operesheni endelevu za kupambana na ugaidi zinazofanywa na jeshi.

"Hivi karibuni, kumekuwa na msukumo mpya kwenye operesheni zetu nchini kote, na kuleta mafanikio ya kupongezwa, haswa kaskazini mashariki," Badaru amesema, bila kueleza muda hasa wa kutekelezwa operesheni hizo dhidi ya ugaidi.

Waziri huyo amesisitiza kuwa, wakati wa kuendeleza mapambano dhidi ya magaidi hao, vikosi vya serikali pia vimeongeza ujasusi wao maradufu ili kuzuia mashambulizi ya wahalifu hao.

Katika nchi jirani ya Niger, wanajeshi wasiopungua10 waliuawa na saba kujeruhiwa katika shambulio la karibuni katika eneo la Dosso kusini mwa nchi. Mamlaka za nchi hiyo zilieleza hayo jana katika taarifa iliyotangazwa kwenye redio ya serikali, huku chanzo kimoja cha usalama kikiiambia Reuters kuwa, yumkini idadi ya askari waliouawa ikawa kubwa zaidi.

Mashambulizi hayo ya kuvizia ya Jumatatu kusini mwa Niger yanaaminika kufanywa na "magaidi" ambapo inaarifiwa kuwa, washambuliaji kadhaa wameuawa pia na wengine kukamatwa katika makabiliano hayo.