Niger katika Mkutano wa UNGA: Ufaransa inapasa kukumbuka na kutambua jinai zake
Lamine Zeine Ali Mahaman Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Niger ameikosoa Ufaransa nchi mkoloni wa zamani wa nchi hiyo akisema kuwa nchi hiyo ya Ulaya inatumia ugaidi kudhoofisha taifa hilo la eneo la Sahel.
Lamine Zeine amesema Paris inapasa kukumbuka na kutambua jinai zake ilizofanya nchini humo tangu mwaka 1899.
"Tangu wanajeshi wa Ufaransa wafurushwe Niger mwaka 2023, serikali ya Ufaransa imeanzisha mpango wa chini kwa chini wa kuidhoofisha nchi yangu," amedai Mahaman katika hotuba yake kwa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa [UNGA] jana Jumamosi.
Kiongozi wa Niger ameituhumu Ufaransa kuwa inawapa mafunzo, inawafadhili kifedha na kuwapatia silaha magaidi na wakati huo huo inajaribu kuibua mazingira ya kujiri mizozo ya kikabila huko Niger katika eneo la Sahel.
Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Niger amesema kuwa Paris imeanzisha kampeni ya "kuchafua taswira ya Niger inayolenga kuidhoofisha nchi hiyo, taasisi zake, viongozi wa kisiasa na kijeshi.
Mahaman ameuambia Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba Ufaransa imekuwua ikichochea "mvutano wa kisiasa kati ya Niger na baadhi ya majirani zake," na kwamba Paris inazuia miradi ya maendeleo ya Niger na kupiga kura dhidi ya nchi hiyo katika taasisi za fedha.