Polisi 10 wauawa katika shambulio kwenye kituo cha polisi Niger
-
Polisi wa Niger
Askari polisi wasiopungua 10 wa Niger wameuawa wakati watu wenye silaha waliposhambulia kituo cha polisi kaskazini mwa nchi hiyo. Eneo la kaskazini mwa Niger limekumbwa na machafuko ya magenge ya wahalifu wenye silaha.
Watu wenye silaha walishambulia kituo cha polisi huko Assamaka, mji wa jangwani ulio karibu na mpaka na Algeria. Mji huo unatumiwa kama kituo cha safari za wahamiaji wa nchi za magharibi mwa Afrika kuelekea kaskazini mwa bara hilo.
Wahalifu wawili pia wameuawa katika hujuma hiyo iliyolenga kituo hicho cha polisi cha Niger huko Assamaka.
Shambulizi katika kituo cha polisi cha Niger karibu na mpaka wa Algeria limeripotiwa huku Niger, Mali na Burkina Faso zikikusudia kuimarisha ushirikiano wa kiusalama chini ya kikosi kipya cha pamoja kwa lengo la kupambana na makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel.
Desemba 20 mwaka jana nchi hizo tatu ziliaanzisha rasmi kikosi hicho chenya askari 5,000 kwa lengo la kufanya oparesheni za pamoja dhidi ya ugaidi, kuimarisha usalama katika maeneo ya mipaka na mawasiliano ya kiintelijinsia.
Makao makuu ya kikosi hicho cha pamoja cha Mali, Niger na Burkina Faso yako Niamey, Niger na kinangozwa na Jenerali Daouda Traore wa Burkina Faso.