Aref: Msingi wa kuimarika uhusiano wa Iran, Niger ni Mapinduzi ya Kiislamu
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran, Mohammad-Reza Aref amesema Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikitekeleza sera yake ya kukuza uhusiano na Niger na mataifa mengine ya bara la Afrika kwa kuzingatia thamani na maadili ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Aref aliyasema hayo jana Jumanne alipokutana na Waziri wa Mafuta wa Niger, Sahabi Oumarou, ambaye yupo Tehran, akiongoza ujumbe wa nchi yake katika Mkutano wa Tatu wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Iran na Afrika.
Amesema serikali ya sasa wa Iran ina azma ya dhati ya kuendeleza uhusiano wa pande mbili na mataifa ya Afrika ikiwemo Niger katika maeneo yenye maslahi ya pamoja. "Kuwepo kwa maafisa wakuu wa Niger kwenye mkutano huo wa kilele pamoja na kamisheni ya pamoja ni hatua ya matumaini ya kuboresha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili," ameongeza.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesisitiza kwamba, kuimarisha uhusiano na Niger ni kipaumbele, "kutokana na msimamo wake kuhusu maendeleo ya kikanda na kimataifa pamoja na mtazamo wa pamoja kuhusu masuala ya Palestina na Lebanon."
Akijibu wito wa waziri wa Niger wa kuimarishwa uhusiano katika kilimo, mafuta na nishati endelevu, Aref alitaja maeneo haya matatu kama vipaumbele vya uhusiano wa Iran na Niger, ambayo alisema yatachunguzwa na tume ya pamoja.
Akizungumzia mahusiano ya kiuchumi, Makamu wa Rais wa Iran amesema kuwa sekta binafsi ya nchi hizi mbili inapaswa kufanya kazi katika miradi ya pamoja na uwekezaji ili kusukuma ushirikiano katika kiwango cha juu zaidi.
Katika kikao hicho, Waziri wa Mafuta wa Niger, Sahabi Oumarou sanjari na kutoa salamu za rambirambi kwa tukio hilo la kusikitisha la mripuko katika Bandari ya Shahid Rajaee, amesema kuwa nchi yake inaona fahari kualikwa kuhudhuria Mkutano wa Kilele wa Iran na Afrika na Maonyesho ya 2025.