Sep 27, 2024 03:04 UTC
  • Mali, Burkina Faso, Niger zamchunguza mwanahabari wa France 24

Waendesha mashtaka katika nchi zinazoongozwa na serikali za kijeshi za Mali, Burkina Faso na Niger wameanzisha uchunguzi dhidi ya mwandishi wa habari wa Ufaransa Wassim Nasr, wakimtuhumu kuwa "mshirika wa ugaidi" kutokana na uchambuzi wake juu ya mashambulizi ya magenge ya kigaidi.

Nasr ambaye anafanya kazi na shirika la utangazaji la France 24, na mchambuzi wa masuala ya usalama mara kwa mara amekuwa anatoa tathmini na maoni yake kuhusu ugaidi uliokita mizizi nchini Mali mwaka 2012, na kuenea katika nchi nyingine za eneo la Sahel la Afrika Magharibi.

Waendesha mashtaka kutoka idara za mahakama zinazohusika na ugaidi nchini Mali, Burkina Faso na Niger wote walitoa taarifa ya pamoja, iliyorushwa kwenye runinga zao za kitaifa siku ya Jumatano.

Wanamshutumu Nasr kwa kutoa maoni ambayo "ni sawa na vitendo vya wazi vya utangazaji na uungaji mkono" kwa shughuli za kigaidii, wakirejelea shambulio la hivi karibuni huko Bamako na shambulio la 2023 katika mji wa Burkina Faso wa Djibo.

Huko nyuma pia, Mali ilichukua hatua ya kusimamisha nchini humo matangazo ya Redio ya Kifaransa ya RFI na televisheni ya France 24 na TV5 Monde kwa muda wa miezi kadhaa, kufuatia ukiukaji wa Sheria ya Udhibiti wa Vyombo vya Habari, na kwa kuripoti habari za uwongo kwamba jeshi linaua raia.

Kadhalika serikali za Niger na Burkina Faso zimewahi kusimamisha matangazo ya RFI na France 24 zinazofadhiliwa na serikali ya Paris, kwa madai ya kutangaza habari za uwongo na upotoshaji.

Tags