Oct 04, 2024 07:12 UTC
  • Niger yasimamisha kipindi cha Wafaransa kinachodhalilisha wanawake Waafrika

Serikali ya kijeshi ya Niger imepiga marufuku kipindi kinachorushwa na kanali ya televisheni ya Ufaransa ikisisitiza kuwa kipindi hicho ni tishio kwa thamani za nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Baraza Kuu la Mawasiliano la Niger limesema katika taarifa kuwa, limepiga marufuku kipindi cha 'The Bachelor' kilichokuwa kinarushwa hewani na televisheni ya Canal Plus ya Ufaransa, likieleza kuwa kinamdhalilisha na kumnyanyapaa mwanamke wa Kiafrika. 

Limeeleza bayana kuwa, filamu hiyo haizingatii mipaka wala kulinda kizazi cha vijana wa taifa hilo la magharibi mwa Afrika. Baraza Kuu la Mawasiliano la Niger limesema limepiga marufuku kipindi hicho kwa kuwa kinaeneza na kushajiisha masuala ya ufuska, jambo ambalo linakanyaga thamani, tamaduni, mila na desturi za nchi hiyo.

Huko nyuma pia, serikali ya Niger imewahi kusimamisha nchini humo matangazo ya radio ya Kifaransa ya RFI na televisheni ya France 24 zinazofadhiliwa na serikali ya Paris, kwa madai ya kutangaza habari za uwongo na upotoshaji.

Haya yanajiri siku chache baada ya serikali ya kijeshi ya Mali kupiga marufuku kanali ya televisheni ya Ufaransa ya LCI kurusha matangazo yake kwa muda wa miezi miwili kutokana na kile kilichotajwa kuwa upotoshaji kuhusu hali ya usalama wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Tags