Serikali ya Niger: Raia waliouawa katika mashambulio ya wabeba silaha hawapungui 137
Serikali ya Niger imetangaza kuwa, raia waliouawa katika hujuma za kinyama zilizofanywa na washambuliaji waliobeba silaha katika vijiji kadhaa vya eneo la Tahoua kusini magharibi mwa nchi hiyo hawapungui 137.
Wakati taarifa iliyotolewa awali na viongozi wa eneo hilo ilieleza kuwa watu wasiopugua 60 waliuawa katika shambulio hilo la Jumapili, msemaji wa serikali Zakaria Abdourahamane ameeleza katika taarifa aliyotoa hapo jana kupitia televisheni ya taifa kuwa, watu wasiopungua 137 waliuawa katika shambulio hilo kubwa zaidi la umwagaji damu kuwahi kushuhudiwa nchini humo kwa miaka kadhaa sasa.
Kwa mujibu wa afisa mmoja wa Tahoua, watu hao waliokuwa wamebeba silaha wakiwa wamepanda mapikipiki walivishambulia vijiji vya Intazayene, Bakorat na Wistane vilivyoko karibu na mpaka wa nchi hiyo na Mali na kufyatulia risasi "kila kilichokuwa kikitembea" .
Zakaria Abdourahamane ameongeza kuwa, majambazi hao wanaofanya mauaji, sasa wamewafanya raia kuwa walengwa wakuu na kwenda mbali zaidi kwa kueneza vitisho na ukatili.
Rais mpya wa Mali Mohamed Bazoum, ambaye ushindi wake katika uchaguzi wa marudio uliofanyika mwezi uliopita ulithibithishwa rasmi na mahakama ya juu ya nchi hiyo siku ya Jumapili amelaani mauaji hayo ya raia akiyaita kuwa ni ya "kishenzi".
Niger, ambayo kwa mujibu wa vigezo vya maendeleo vya Umoja wa Mataifa, ndiyo nchi masikini zaidi duniani inajaribu kupambana na hujuma za utumiaji silaha zilizosambaa ndani ya nchi hiyo kutokea Mali na Nigeria na kusababisha mamia ya watu kuuuawa na kuwaacha wengine wanaokaribia nusu milioni bila makazi.../