Zimbabwe yapiga marufuku kuingiza magari ya zaidi ya miaka 10 nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i68608-zimbabwe_yapiga_marufuku_kuingiza_magari_ya_zaidi_ya_miaka_10_nchini_humo
Zimbawe imepiga marufuku kuingiza nchini humo magari makongwe yaliyotengenezwa zaidi ya miaka 10 iliyopita ikiwa ni hatua ya kukuza viwanda vya ndani, kupunguza gharama na kukabiliana na uchafuzi wa mazingira na hali ya hewa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 03, 2021 07:20 UTC
  • Zimbabwe yapiga marufuku kuingiza magari ya zaidi ya miaka 10 nchini humo

Zimbawe imepiga marufuku kuingiza nchini humo magari makongwe yaliyotengenezwa zaidi ya miaka 10 iliyopita ikiwa ni hatua ya kukuza viwanda vya ndani, kupunguza gharama na kukabiliana na uchafuzi wa mazingira na hali ya hewa.

Marufuku hiyo ilianza kutekelezwa jana Ijumaa. Kwa mujibu wa marufuku hiyo, magari yote makongwe yenye zaidi ya miaka 10 yamepigwa marufuku kuingizwa nchini Zimbabwe isipokuwa magari ya biashara na yanayotumika kwa ajili ya kilimo.

Wakosoaji wanasema kuwa, kuingizwa magari ya mitumba kunachangia sana ajali za barabarani, kunazidisha hewa chafu na kunavuruga juhudi za kuimarisha viwanda vya ndani pamoja na jitihada za kulinda mazingira.

Sheria hiyo mpya pia inatarajiwa kutia nguvu viwanda vya ndani na kuvipa motisha wa kudhamini mahitaji ya ndani ya nchi bila ya kutegemea bidhaa kutoka nje.

Mwaka jana Waziri wa Fedha wa Zimbabwe, Mthuli Ncube alitangaza kwamba nchi hiyo itaanza kutengeneza yenyewe mabasi ya usafiri wa umma ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kuirejesha nchi katika kilele cha uzalishaji mkubwa wa magari.