Ethiopia: File na bwawa la Renaissance si kadhia ya kimataifa
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ethiopia amepinga mpango wowote wa kulifanya suala la bwawa la Renaissance kuwa mgogoro wa kimataifa.
Demeke Mekonnen amesema kuwa, Addis Ababa haitasalimu amri mbele ya mashinikizo yanayoitaka ikubali makubaliano ya kikoloni kuhusu maji ya Mto Nile.
Mekonnen ameongeza kuwa, tatizo la bwawa la Renaissance litapatiwa ufumbuzi kupitia mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Afrika "iwapo Misri na Sudan zitafuata njia sahihi".
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ethiopia amesema kuwa, nchi yake haitakubali masharti yasiyo ya kiadilifu yanayotumiwa na Misri na Sudan kwa ajili ya kuendeleza udhibiti wa maji ya Mto Nile.
Ethiopia inasisitiza kuwa itatekeleza awamu ya pili ya kujaza maji katika bwawa na Renaissance mwezi Julai mwaka huu, hata kama hakutafikiwa mapatano baina ya nchi hizo tatu zinazozozana kuhusiana na ujenzi wa bwawa hilo.
Katika upande mwingine Cairo na Khartoum zinasisitiza kuwa, kuna ulazima wa kufikiwa mapatano baina ya pande hizo tatu kabla ya kuanza awamu ya pili ya kujaza maji katika bwawa la Renaissance na kuanza kazi bwawa hilo.
Misri na Sudan zinasema ujenzi wa bwawa hilo ambalo limegharimu karibu dola bilioni nne, utapunguza maji ya nchi hizo na hivyo kuvuruga maisha ya mamilioni ya watu. Ethiopia nayo inasisitiza kuwa ujenzi wa bwawa hilo ni muhimu kwa ajili ya kueneza umeme katika nchi hiyo ili kuimarisha sekta ya viwanda na pia kuuza bidhaa hiyo katika nchi za nje.
Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri kutishia kwamba "Cairo itatoa jibu lisilotasawarika iwapo nchi yake itapata madhara kutokana na bwana la Renaissance linalojengwa na Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile."
Rais wa Misri alisisitiza kuwa maji ya Misri ni mstari mwekundu na anayetaka kujaribu atakiona cha mtemakuni.