Watu 19 wauawa katika shambulio la wabeba silaha nchini Niger
(last modified Mon, 19 Apr 2021 07:46:16 GMT )
Apr 19, 2021 07:46 UTC
  • Watu 19 wauawa katika shambulio la wabeba silaha nchini Niger

Kwa akali watu 19 wanaripotiwa kuuawa katika shambulio la wabeba silaha huko magharibi mwa Niger,mpakani mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika na Mali.

Gavana wa jimbo la Tillaberi, Ibrahim Tidjani Katiella amenukuliwa akisema yumkini waliotekeleza shambulio hilo waliingia kinyemela nchini humo wakitokea Mali. Hakuna kundi liilotangaza kuhusika na hujuma hiyo.

Afisa mmoja wa Manispaa ya Dessa ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, wavamizi hao huku wakiwa wamefuka nyuso zao na wakiwa juu pikipiki walishambulia kijiji cha Gaigarou usiku wa kuamkia jana na kuanza kufyatua risasi ovyo.

Amesema wavamizi hao waliushambulia mkusanyiko wa wanakijiji waliokuwa wamejumuika kwa ajili ya mazishi, na kisha wakaaza kumpiga risasi kila aliyekuwa mbele yao. Watu kadhaa wamejeruhiwa pia katika shambulio hilo.

Genge la wabeba silaha Niger

Hii ni katika hali ambayo, mwishoni mwa mwezi uliopita, serikali ya Niger ilitangaza kuwa, raia waliouawa katika hujuma za kinyama zilizofanywa na washambuliaji waliobeba silaha katika vijiji kadhaa vya eneo la Tahoua kusini magharibi mwa nchi hiyo hawapungui 137.

Kundi la kigaidi la Boko Haram lilishika silaha mwaka 2009 kwa lengo la kile lilichotaja kuwa, kuwa huru eneo la kaskazini mwa Nigeria; na kuanzia hapo likaanza kueneza jinai na mashambulizi yake huko Niger, Chad na kaskazini mwa Cameroon. Tangu wakati huo hadi sasa kundi hilo limeua watu wapatao 36 elfu na kusababisha raia wengine zaidi ya milioni mbili pia kuwa wakimbizi katika nchi hizo za magharibi mwa Afrika.

Tags