Apr 27, 2021 06:45 UTC
  • Misri yawanyonga watuhumiwa wa uvamizi dhidi ya kituo cha polisi, Amnesty yalaani

Idara ya Magereza ya Misri inayoongozwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi hiyo imetangaza kuwa, imetekeleza hukumu ya kifo dhidi ya watu 9 waliohukumiwa kwa hatia ya kile kinachotajwa kuwa ni uvamizi dhidi ya kituo cha polisi.

Taarifa iliyotolewa na idara hiyo imesisitiza kuwa, hukumu hiyo ilitekelezwa jana katika Gereza la Wadi el-Natrun na kwamba familia za wafungwa hao zimetakiwa kwenda kuchukua maiti zao. 
Mahakama ya Jinai ya Cairo ilikuwa imewahuku kifo watuhumiwa 20 wakihusishwa na tukio hilo la kuvamia kituo cha polisi cha Kerdasa mwaka 2013. 

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International litangaza kuwa, kunyongwa kwa watuhumiwa hao wa kadhia ya uvamizi wa kituo cha polisi cha Kerdasa ni ushahidi wa kutisha unaoonyesha jinsi serikali ya Misri isivyojali haki ya kuishi ya raia wake na ukiukaji wake wa sheria za kimataifa.

Misri inakosolewa sana kwa kuendelea kuwanyonga wapinzani

Taarifa ya Amnesty International imesema kunyongwa watuhumiwa hao katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kunaonyesha kuwa serikali ya Cairo imeazimia kuendelea kutumia adhabu ya kifo kwa kiasi kikubwa. Imesema watu hao wamenyongwa kupitia kesi isiyo ya kiadilifu na kwa kutumia ushahidi uliopatika kwa kuwatesa watuhumiwa. 

Taasisi nyingine kadhaa za kutetea haki za binadamu za ndani na nje ya Misri zinasema kuwa, watu 17 walinyongwa jana nchini Misri wakiwemo wapinzani kadhaa wa serikali ya Cairo.  

Tags