Jun 19, 2021 12:34 UTC
  • WHO: Tunatazamia Guinea itangaze mwisho wa mripuko wa Ebola

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema anatarajia kuwa serikali ya Guinea itatangaza leo Jumamosi habari ya kudhibitiwa mripuko wa hivi sasa wa ugonjwa wa Ebola nchini humo.

Katika kikao na waandishi wa habari, Dakta Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, "Guinea imefanikiwa kudhibiti mripuko huo katika kipindi cha miezi minne, na kuzuia usienee nje ya mipaka yake."

Mkuu huyo wa WHO amesema watu zaidi ya 11,000 wamepigwa chanjo ya Ebola ndani ya muda huo nchini Guinea Conackry.

Februari mwaka huu, Guinea Conakry ilizindua zoezi la utoaji chanjo ya kukabiliana na ugonjwa hu hatari wa Ebola. Mgonjwa wa kwanza wa Ebola nchini Guinea kwa mwaka huu alibainika tarehe 14 mwezi Februari na hadi sasa makumi wamebainika kuambukizwa maradhi hayo, kati yao hao 12 wamefariki dunia. 

Mripuko huo wa Ebola ulioripotiwa nchini Guinea ni wa kwanza kuiathiri nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika tangu ule wa mwaka 2013 hadi 2016 uliouwa watu zaidi ya 11,300 katika nchi hiyo pamoja na Liberia na Sierra Leone. 

Kampeni ya chanjo ya Ebola

Ebola inasababisha homa kali mwilini na pale mtu anapozidiwa husababisha kuvuja damu mfululizo. Homa ya Ebola pia inaambukizwa kupitia mtu kugusa majimaji kutoka katika mwili wa mgonjwa. Aidha watu wanaoishi na kuwahudumiwa wagonjwa hao wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa. 

Kabla ya kuripotiwa nchini Guinea Conakry, kesi nyingine za Ebola tayari zilikuwa zimeripotiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hata hivyo mwezi uliopita wa Mei, Shirika la Afya Duniani lilitangaza kumalizika mripuko huo wa 12 wa Ebola nchini DRC.

Tags