Jan 11, 2023 11:15 UTC
  • Uganda yatangaza kumalizika kwa mlipuko wa Ebola ulioua makumi

Uganda imetangaza habari ya kudhibitiwa na kutokomezwa mlipuko wa Ebola ambao umeua makumi ya watu nchini humo tangu Septemba mwaka uliomalizika 2022.

Tangazo hilo limetolewa leo Jumatano na Jane Ruth Aceng, Waziri wa Afya wa Uganda katika hafla ya kuadhimisha mwisho wa mlipuko wa maradh hayo hatarishi.

Dakta Aceng amebainisha kuwa, 'Tumefanikiwa kudhibiti msambao wa Ebola nchini Uganda." Tangazo hilo la Jumatano limekuja baada ya Uganda kutoripoti kesi yoyote mpya ya ugonjwa huo ndani ya siku 42 zilizopita, kwa kuzingatia miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus ameipongeza Uganda kwa kufanikiwa kuudhbiti mlipuko wa Ebola. Uganda imetokomeza Ebola pasi na kuwepo chanjo iliyoidhinishwa kwa ajili ya spishi ya maradhi hayo iliyoripotiwa katika mlipuko wa sasa. 

Takwimu za Wizara ya Afya ya Uganda zinaonesha kuwa, watu 55 wamefariki dunia kwa maradhi hayo katika mlipuko huu ulioisha, wakiwemo wahudumu sita wa afya; huku kesi 143 zikinakiliwa katika muda huo wa miezi minne.

Hapo awali Ahmed Ogwell Ouma, Mkuu wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (AFRICA CDC) aliipongeza serikali ya Uganda kwa jinsi ilivyochukua hatua bora za kuzuia kuenea kwa virusi hivyo, akisema ilichukua takriban siku 70 kudhibiti hali hiyo.

Tags