Mahakama ya ICC yathibitisha mashtaka dhidi ya Joseph Kony
-
Kony
Majaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC yenye makao yake mjini Hague, Uholanzi wamethibitisha kuwa kiongozi wa waasi wa Uganda Joseph Kony anakabiliwa na mashtaka ya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu na hivyo kufungua njia kwa ajili kuanza kesi yake iwapo tu atatiwa nguvuni.
Jopo la majaji watatu wa ICC liliamua kuwa kuna "sababu kubwa" za kuamini kwamba Kony anahusika na makosa 29 ya ukatili, ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji na vitendo vya kudhaliishaji kingono alivyofanya wakati akiongoza kundi kwa jina la Lord's Resistance Army, kundi la waasi lililofanya ugaidi kaskazini mwa Uganda na baadaye katika maeneo mbalimbali ya katikati mwa Afrika.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya mjini Hague Uholanzi imethibitisha mashtaka haya yanayomkabili Kony ikiwa imepita karibu miongo miwili baada ya mahakama hiyo kutoa kibali cha kukamatwa kwake.
Mame Mandiaye Niang Naibu Mwendesha Mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ameeleza kuwa uhalifu uliofanywa na kundi la LRA umeacha makovu kwa jamii mbalimbali na kwamba "utamaduni wa jamii ya Kaskazini mwa Uganda umesambaratika na bado unajitahidi kujijenga upya."
ICC imesikiliza kesi hiyo kwa mara ya kwanza bila ya mtuhumiwa kuwepo mahakamani. Joseph Kony alijizolea umaarufu duniani mwaka 2012 baada ya kusambaa kwa taarifa katika mitandao ya kijamii zilizoangazia tuhuma zinazomkabili. Kiongozi huyo wa waasi wa LRA hadi sasa hajatiwa nguvuni licha ya juhudi kubwa za kimataifa.