Jumanne, tarehe 11 Novemba, 2025
Leo ni Jumanne tarehe 20 Jamadil Awwal 1447 Hijria mwafaka na tarehe 11 Disemba 2025.
Siku kama ya leo miaka 765 iliyopita inayosadifiana na tarehe 20 Jumadil Awwal 682 Hijria, alizaliwa Muhammad bin Hassan Hilli mwenye lakabu ya Fakhrul Muhaqqiqiin katika mji wa Hilla nchini Iraq.
Muhaqqiq Hilli alibobea na kutabahari kwenye elimu za Tafsiri ya Qur’ani, Fiqh na Usulul Fiqh. Mwanachuoni huyo alipata elimu ya kidini kutoka kwa mzazi wake, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake.
Fakhrul Muhaqqiqiin ameandika vitabu vingi miongoni mwavyo ni "Sharh Mabadiul Usul", "Tahswilul Najat" na “al Kaafiyah”. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 771 Hijria.

Katika siku kama ya leo miaka 710 iliyopita yaani tarehe 20 Jamadil Awwal mwaka 737 alifariki dunia faqihi wa Kiislamu Abu Abdullah Muhammad ibn Hajj al-Abdari al-Fasi mashuhuri kwa jina la Ibnul Hajj. Al Fasi awali alipata elimu kwa maulamaa wa mji wa Fas huko Morocco ya leo.
Baadaye alielekea Cairo na kuishi huko hadi mauti yalipomfika. Faqihi Abu Abdullah al Fasi ameandika vitabu vingi vya thamani kikiwemo kile cha al Mad-khal. Katika kitabu hicho, Ibn Hajj amechunguza masuala mbalimbali yakiwemo ya kiakhlaqi, kifiqi, kijamii na kiuchumi.

Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, Vita vya Kwanza vya Dunia vilifikia tamati baada ya kutiwa saini mkataba wa kuacha vita hivyo.
Vita vya Kwanza vya Dunia vilipiganwa kuanzia mwaka 1914 hadi 1918 kati ya nchi waitifaki yaani serikali za Russia, Uingereza, Ufaransa na Italia kwa upande mmoja, na nchi za Ujerumani, Bulgaria, Utawala wa Othmania na ufalme wa Austria na Hungary kwa upande wa pili. Watu zaidi ya milioni 15 waliuawa katika vita hivyo na wengine milioni 20 kujeruhiwa.
Vilevile vilisababisha hasara inayokadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 150 kwa nchi zilizopigana vita hivyo.

Katika siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, virusi vinavyosababisha maradhi hatari ya kupooza viungo vya miili ya watoto yaani Polio, viligunduliwa.
Virusi hivyo vilipewa jina la virusi vinavyolemaza watoto kwa sababu ya kuwashambulia zaidi watoto wadogo na kuwapoozesha viungo vyao vya mwili. Baadaye kidogo mwanasayansi Dakta Jonas Salk aliyegundua virusi vya Polio alifanikiwa pia kugundua chanjo yake.
Miaka 50 iliyopita katika siku kama ya leo, Angola ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno.
Wakoloni wa Kireno kwa mara ya kwanza waliingia katika ardhi ya Angola mwaka 1483 Miladia. Wakati huo, ardhi ya Angola ilikuwa sehemu ya ufalme wa Kongo, Zaire ya zamani. ***
Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, aliaga dunia Yasser Arafat Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kiongozi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) katika hospitali moja mjini Paris, Ufaransa.
Alizaliwa mwaka 1929 na kuanza harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Israel akiwa katika rika la ujana. Mwaka 1946, Yasser Arafat alielekea nchini Misri kwa ajili ya masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Cairo na miaka mitano baadaye alihitimu masomo katika taaluma ya Usanifu Majengo.
Mwaka 1965 alirejea Palestina na kuasisi Harakati ya Fat-h ili kupambana na utawala wa Tel Aviv. Miaka minne baadaye alichukua hatamu za kuongoza PLO hadi alipoaga dunia.