Mgombea urais Uganda: Nilipigwa na askari usalama
-
Bob Wine, mgombea urais nchini Uganda
Bob Wine au Robert Kyagulanya mgombea kiti cha urais nchini Uganda kwa tiketi ya chama cha upinzani cha NUP amesema kuwa askari usalama wa nchi hiyo wampiga yeye na wafuasi wake wakati walipokuwa katika kampeni za uchaguzi kaskazini mwa nchi hiyo katika kile kinachotajwa kuwa muendelezo wa ghasia na utumiaji mabavu unaoshuhudiwa Uganda kabla ya uchaguzi wa Rais Januari 15 mwakani.
Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi ambaye awali alikuwa mwamuziki na sasa amegeukia siasa anachuana kwa mara ya pili na Rais sasa wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni aliye na miaka 81 baada ya kushika nafasi ya pili katika uchaguzi wa rais mwaka 2021.
Katika msururu wa machapisho aliyotuma kwenye akaunti yake ya X; Bob Wine amesema alipigwa na fimbo usoni na kwamba wafuasi wake wengine pia walipigwa hadi kulazwa hospitalini. Walikumbana na vipigo vya askari usalama walipokuwa wakikaribia ukumbi wa kampeni huko Gulu, jiji kubwa zaidi kaskazini mwa Uganda.
"Wahalifu waliovalia sare za polisi na kijeshi walitushambulia kwa fimbo na mawe na kuanza kuwapiga watu wetu,"ameandika Robert Kyagulanyi katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X.
Wakati huo huo Chris Magezi Msemaji wa Polisi ya Uganda amemtuhumu mgombea huyo wa kiti cha urais kwa kuitisha maandamano haramu na kufanya kampeni zaidi ya muda ulioainishwa. "Vikosi vya usalama vipo kuhakikisha kila mtu anafuata sheria," amesema Msemaji wa Polisi ya Uganda.
Volker Turk Mku wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Jumatano iliyopita alikosoa kile alichokitaja kama "ukandamizaji wakupindukia" dhidi ya upinzani nchini Uganda na kusema wafuasi wasiopungua 550 wa chama cha Wine cha National Unity Platform wametiwa mbaroni mwaka huu.