Tume ya Uchaguzi Uganda: Museveni aongoza kwa asilimia 61.7 ya kura
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135538-tume_ya_uchaguzi_uganda_museveni_aongoza_kwa_asilimia_61.7_ya_kura
Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Uganda yanaonyesha kuwa Rais Museveni ameibuka na asilimia 61.7 ya kura halali zilizohesabiwa hadi sasa.
(last modified 2026-01-16T07:14:54+00:00 )
Jan 16, 2026 07:14 UTC
  • Yoweri Museveni
    Yoweri Museveni

Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Uganda yanaonyesha kuwa Rais Museveni ameibuka na asilimia 61.7 ya kura halali zilizohesabiwa hadi sasa.

Mwenyekiti wa hiyo Simon Mugenyi Byabakama ametangaza matokeo haya ya awali kwa vyombo vya habari, matokeo ambayo yanatoa ishara ya kuendelea utawala wa miongo minne wa Rais Museveni.

Byabakama ametangaza kuwa: Yoweri Tibuhaburwa Kaguta Museveni wa chama awala cha NRM hadi sasa  amepata  kura 14,232, ambazo ni sawa na asilimia 61.7 ya kura halali zilizopigwa hadi sasa. Jumla ya kura halali kwa wagombea wote hadi sasa ni 23,049. Kura batili hadi sasa ni 796, ambazo ni sawa na asilimia 3.34 ya kura zote zilizopigwa.

Matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu wa Uganda yanatarajiwa kutolewa ndani ya masaa 48 baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika.

Mshindani mkuu wa Museveni katika kinyanganyiro cha kiti cha urais mwanamuziki aliyegeuka mwanasiasa Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine mwenye umri wa miaka 43 ambaye amewakilisha kizazi kinachotaka mabadiliko ya kisaisa nchini Uganda amepata asilimia 33.64 ya kura kwa mujibu wa matokeo ya Tume ya Uchaguzi.  Kyagulanyi amedai kufanyika udanganyifu katika uchaguzi wa rais. 

Vituo vya kupigia kura vilifungwa Alhamisi jioni kote nchini Uganda baada ya uchaguzi kufanyika licha ya kasoro mbalimbali kushuhudiwa, ikiwa ni pamoja na matatizo ya kiufundi, vituo kuchelewa kufunguliwa, masunduku ya kura kutowasili kwa wakati, kuzimwa mtandao wa intaneti hali ilisababisha pia mitambo ya upigaji kura kwa njia ya kielektroniki kushindwa kufanya kazi ipasavyo.