CIA ilitoa taarifa zilizopelekea kukamatwa Shujaa Mandela mwaka 1962 huko Durban
Hayati Shujaa Nelson Mandela wa Afrika Kusini alikamatwa na utawala wa makaburu mwaka 1962 kufuatia taarifa za siri zilizotolewa na shirika kuu la kijasusi la Marekani, CIA.
Maelezo hayo yamefichuliwa na jasusi wa zamani wa CIA Donald Rickard, muda mfupi kabla hajaaga dunia.
Alipokamatwa, Mandela alitumikia kifungo cha miaka 27 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kuendesha mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi. Aliachiliwa huru mwaka 1990 na kisha baada ya hapo kuchaguliwa kuwa rais wa kwanza mweusi Afrika Kusini.
Taarifa hiyo iliyochapishwa na gazeti la Sunday Times la London imethibitisha nadharia ya muda mrefu kuwa Mandela alikuwa akifuatiliwa kwa karibu na majasusi wa CIA wakati akipigania ukombozi wa Afrika Kusini. Rickard, ambaye alifichua taarifa hiyo mapema mwaka huu, alikuwa akifanya kazi kama mwanadiplomasia Afrika Kusini ingawa hakujitambulisha rasmi kama jasusi wa CIA.
Nchi za Magharibi zilimtazama shujaa Mandela kama mkomunisti na tishio ingawa daima alikataa kuwa mwanachama wa chama cha kikomunisti.
Ikumbukwe kuwa Mandela ambaye alikuwa Rais wa Afrika Kusini kutoka mwaka 1994 hadi 1999 alikuwa katika orodha ya magaidi Marekani hadi mwaka 2008.
Aidha kwa muda mrefu Marekani ilikitazama chama tawala cha Afrika Kusini ANC, ambacho kilipigania ukombozi wa nchi hiyo, kama chama cha kigaidi.