Italia yakanusha madai ya kutaka kuimarisha uwepo wa askari wake Libya
Wizara ya Ulinzi ya Italia imekadhibisha madai ya baadhi ya vyombo vya habari kuwa Rome ina mpango wa kuongeza idadi ya wanajeshi wake nchini Libya.
Katika taarifa, wizara hiyo imekanusha madai kuwa inafanya mazungumzo na maafisa wa Libya juu ya suala la nchi hiyo ya Ulaya kupanua uwepo wa askari wake katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Wizara ya Ulinzi ya Italia imeyataja madai hayo yaliripotiwa na vyombo vya habari hususan vya Italia kuwa propaganda na kusisitiza kuwa hayana msingi wowote. Magazeti ya Italia hivi karibuni yalisema Rome inapanga kushirikiana na Ufaransa kutuma askari 600 zaidi nchini Libya.
Hii ni katika hali ambayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, Najla al-Manqoush ametoa mwito kwa nchi zote ajinabi kuviondoa vikosi vyao katika hiyo ya Kiarabu ambayo inakabiliwa na mapigano tokea mwaka 2011.
Kadhalika kongamano kuhusu amani ya Libya lililofanyika Berlin Ujerumani na ambalo limewashirikisha wawakislishi wa nchi 16 na mashirika manne ya kimatifa, limesisitiza juu ya udharura wa kuondolewa askari wote wa kigeni walioko Libya na kuandaliwa uwanja wa kufanyika uchaguzi mkuu ifikapo Disemba mwaka huu.
Uwepo wa nchi za kigeni katika ardhi ya Libya na hasa uungaji mkono wao kwa makundi ya wanamgambo na hasa wa kusini mwa nchi, umevuruga hali ya mambo nchini na hivyo kufanya utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo kuwa mgumu zaidi.