RSF yalaani kukamatwa waandishi habari nchini Ethiopia, yaamuru waachiwe huru
Jumuiya ya Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RSF) imelaani kile ilichokiita "kukamatwa kwa umati" kwa waandishi wa habari 12 wa Ethiopia ambao walitiwa nguvuni ili "kuwazuia kuchunguza kwa uhuru mzozo unaoendelea katika eneo la Tigray".
RSF imetoa wito wa kuachiwa huru mara moja waandishi hao wa habari.
Taarifa iliyotolewa na shirika hilo imesema kuwa, waandishi wengi wa habari walikamatwa nchini Ethiopia mnamo Juni 30 huko Addis Ababa. Imesema kuwa serikali haikutoa sababu yoyote ya kukamatwa kwa waandishi hao hadi Julai 2, wakati polisi ilipotangaza kuwa, waandishi hao wa habari wamekamatwa kwa kuwa na uhusiano na "kikundi cha kigaidi" kilichopigwa marufuku hivi karibuni na Bunge la Ethiopia cha Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF).
Serikali ya Ethiopia ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya eneo la Tigray Novemba mwaka jana, kwa madai kuwa wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) wamelishambulia jeshi la nchi hiyo na kuwaua askari waliokuwa wamelala na kupora zana zao za kijeshi.
Arnaud Frogh, afisa wa Shirika la Wanahabari Wasio na Mipaka barani Afrika amesema: "Tunalaani kukamatwa kwa umati waandishi wa habari, ambako ni wazi kuwa, kunalenga kuwazuia kufanya uchunguzi wa kujitegemea kuhusu mzozo katika eneo la Tigray."
Mwisho wa wiki iliyopita, Tume ya Haki za Binadamu ya Ethiopia - ambayo ni chombo huru - ilielezea wasiwasi wake mkubwa juu ya kukamatwa waandishi wa habari, ikisisitiza kwamba mahabusu hao wamenyimwa haki ya kukutana na wanasheria na familia zao.
Serikali ya Ethiopia iliweka masharti magumu kwa waandishi wa habari ambao wanafuatilia mzozo na mapigano katika eneo la Tigray.
Kwa sasa Ethiopia inashika nafasi ya 101 kati ya nchi 180 katika viwango vya uhuru wa vyombo vya habari vya Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka.