Umoja wa Afrika watoa wito wa kurejeshwa amani na utulivu Afrika Kusini
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, amelaani kwa nguvu zote vurugu na machafuko makubwa yanayoendelea nchini Afrika Kusini baada ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma kufungwa jela miezi 15 kwa tuhuma za kuhusika na ufisadi na utumiaji mbaya wa madaraka yake.
Moussa Faki Mahamat amekemea vikali machafuko hayo ambayo amesema yamesababisha vifo vya makumi ya raia na matukio ya kutisha ya uporaji wa mali ya umma na ya kibinafsi, uharibifu wa miundombinu, pamoja na kusimamishwa huduma muhimu katika maeneo mbalimbali ya Afrika Kusini kama Kwazulu-Natal na Gauteng.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika pia ametoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa machafuko hayo na kuwatakia shifaa ya haraka na kamili wale waliojeruhiwa.
Vilevile ametoa wito wa kurejeshwa haraka hali ya utulivu na amani nchini Afrika Kusini sambamba na kuheshimiwa kikamilifu utawala wa sheria. Amesisitiza kuwa, kutofanya hivyo kunaweza kuwa na athari mbaya sio tu nchini Afrika Kusini pekee bali pia kwa kanda nzima ya Kusini mwa Afrika.
Moussa Faki Mahamat pia amesisitiza mshikamano kamili na usioyumba wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Serikali na watu wa Afrika Kusini.

Nchi ya Afrika Kusini imekuwa kwenye ghasia na machafuko makubwa kwa siku kadhaa sasa tangu rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma alipojisalimisha kwa vyombo vya dola na kufungwa jela kwa tuhuma za ufisadi.
Wiki iliyopita Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini iliagiza Zuma afungwe jela kwa kukataa kutoa ushahidi katika uchunguzi wa ufisadi uliofanyika katika kipindi chake cha uongozi kutoka 2009 hadi 2018.
Idadi ya watu waliouawa katika ghasia na uporaji nchini Afrika Kusini hadi kufikia jana Jumanne imeongezeka na kufikia watu 72.
Vyombo vya usalama nchini humo vinasema kwamba vurugu na uporaji vimeenea katika majimbo ya Mpumalanga na Cape Kaskazini, baada ya majimbo ya KwaZulu-Natal na Gauteng.
Jacob Zuma alilazimika kujiuzulu mwezi Februari mwaka 2018 kutokana na mashinikizo ya chama tawala cha ANC kwa tuhuma za kuhusika na ufisadi na utumiaji mbaya wa madaraka yake.