Aug 15, 2021 13:28 UTC
  • Ivory Coast yarekodi kisa cha kwanza cha Ebola katika miaka 25

Waziri wa Afya wa Ivory Coast ametangaza kuwa nchi hiyo imesajili kisa cha kwanza cha virusi vya kutokwa na damu vya Ebola ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 25.

Pierre N’Gou Dimba amesema kwenye runinga ya kitaifa ya nchi hiyo kwamba maafisa walithibitisha kesi hiyo baada ya kupima sampuli kutoka kwa mwanamke mwenye umri wa miaka 18 ambaye aliwasili nchini humo kutoka nchi jirani ya Guinea.

Waziri wa Afya wa Ivory Coast amesema: "Hii ni kesi ya pekee na iliyoingizwa nchini kutoka nje, na kwa sasa mgonjwa anapatiwa matibabu katika kitengo cha wagonjwa mahututi mjini Abidjan."

Katika taarifa tofauti, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa kesi hiyo ni maambukizi ya kwanza ya Ebola nchini Ivory Coast tangu 1994.

WHO imesema, habari hii imeripotiwa baada ya Taasisi ya Pasteur huko Ivory Coast kuthibitisha kuwepo ugonjwa wa virusi vya Ebola katika sampuli zilizokusanywa kutoka kwa mgonjwa ambaye alikuwa amelazwa katika mji mkuu wa kibiashara wa nchi hiyo, Abidjan, baada ya kuwasili kutoka Guinea.

WHO imesema uchunguzi wa awali uligundua kuwa mgonjwa huyo alisafiri kwenda Ivory Coast kwa barabara na kwamba aliwasili Abidjan mnamo Agosti 12.

Guinea - iliyokuwa kituo kikuu cha mlipuko wa Ebola wa 2014-2016 -, ilikumbwa tena na virusi vya ugonjwa huo mapema mwaka huu ambao ulitangazwa kumalizika Juni 19.

Mapema wiki hii pia Guinea ilithibitisha kisa cha kwanza cha virusi vya Marburg huko Afrika Magharibi.

 Mtu aliyeambukizwa homa ya Marburg huwa na dalili za maumivu ya kichwa, kutapika damu, maumivu ya misuli na kuvuja damu katika matundu kadhaa ya mwili.

Tags