Makumi ya watu wauawa katika hujuma ya silaha magharibi mwa Niger
Kundi moja la watu wasiojulikana limeua karibu raia 40 huko magharini mwa nchi ya Niger.
Shambulio hilo lilitokea Jumatatu ya jana katika mkoa wa Banibangou eneo lililo karibu na mpaka wa Mali, ambapo wapiganaji wenye silaha wamewaua mamia ya raia mwaka huu pekee.
Mashambulio hayo ni sehemu ya machafuko makubwa yanayoshuhudiwa mara kwa mara katika mipaka ya Mali, Burkina Faso na Niger katika eneo la Sahel barani Afrika ambapo wapiganaji wa makundi ya waasi wanaohusishwa na al Qaeda na Daesh wanataka kulidhibiti eneo hilo.
Tarehe 11 mwezi huu wa Agosti shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lenye makao yake New York huko Marekani liliripoti kuwa, makundi yenye silaha katika maeneo ya Tillabery na Tahoua huko Niger yamewaua raia zaidi ya raia 420 na kuwafukuza makumi ya maelfu ya wengine kutoka kwenye nyumba zao mwaka huu wa 2021 pekee.
Mashambulizi ya makundi ya waasi na magaidi yamepamba moto zaidi mwaka huu nchini Niger. Mnamo mwezi Machi, magaidi waliua watu 137 katika hujuma uliyoratibiwa kenye mkoa wa Tahoua kusini magharibi mwa Niger na mwezi Januari zaidi ya watu 100 waliuawa katika mkoa huo huo kwenye shambulizi la watu waliokuwa na silaha.