Niger: Wanajeshi 16 wauawa katika shambulio la magaidi wa Boko Haram
(last modified Thu, 26 Aug 2021 08:04:21 GMT )
Aug 26, 2021 08:04 UTC
  • Niger: Wanajeshi 16 wauawa katika shambulio la magaidi wa Boko Haram

Wizara ya Ulinzi ya Niger imetangaza kuwa, kwa akali wanajeshi wake 16 wameuawa kufuatia shambulio la kigaidi kusini magharibi mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Niger imeeleza pia kuwa, wanajeshi 16 wameuawa katika shambulio la kundi la kigaidi la Boko Haram katika mkoa wa Diffa na kwamba, makumi ya wengine wamejeruhiwa.

Mauaji ya wanajeshi hao yalitokea baada ya mamia ya wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram kushambulia moja ya kambi za kijeshi kusini mwa nchi hiyo.

Shambulio na mauaji hayo yanatokea siku chache tu baada ya askari wengine 15 wa Niger kuuawa kufuatia shambulio la wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram dhidi yao.

Maeneo mbali mbali ya Niger yamekuwa yakiandamwa na mashambulio ya mara kwa mara ya umwagaji damu ya makundi ya wabeba silaha yenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda na kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS).

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram

 

Genge la kigaidi la Boko Haram lilipanua mashambulizi yake pia hadi katika nchi jirani za Cameroon, Chad na Niger mwaka 2015. 

Hujuma na mashambulio ya kundi la kigadi la Boko Haram yameshaua watu wasiopungua 36,000 na kusababisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya Nigeria hasa katika maeneo yanayopakana na Ziwa Chad.

Tags