Rais Museveni wa Uganda aombwa kupatanisha mizozo ya Sudan Kusini
(last modified Fri, 03 Sep 2021 11:43:44 GMT )
Sep 03, 2021 11:43 UTC
  • Rais Museveni wa Uganda aombwa kupatanisha mizozo ya Sudan Kusini

Shirika la Maendeleo na Tawala za Kieneo (IGAD) limemuomba Rais wa Uganda Yoweri Museveni atumie hekima na uzoefu wake katika masuala ya uongozi ili kusaidia kutatua tatizo la ukosefu wa usalama nchini Sudan Kusini.

Mjumbe wa Sudan Kusini katika jumuiya ya IGAD, Ismail Wais amemuomba Rais Museveni ambaye ameongoza Uganda tangu 1986, aingilie kati na kuipatia Sudan Kusini ushauri kuhusu mbinu za kupata amani.

“Hili eneo linakuhitaji mheshimiwa Rais. Kutokana na uzoefu wako na ushauri wako, Sudan Kusini itakuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama mataifa mengine. Nchi yetu lazima iwe na mabadiliko na tunakuomba utusaidie kwa hili,’ akasema Wais jijini Kampala.

Mjumbe huyo amesema kuwa vita vya kikabila vimelemaza maendeleo nchini Sudan Kusini, na amemtaka Rais Salva Kiir ashirikiane na viongozi wengine wa kimataifa kusaidia ujenzi mpya wa nchi hiyo na kuzima ghasia za kikabila kupitia njia ya mazungumzo.

Sudan Kusini ndiyo taifa changa zaidi Afrika baada ya kujitenga na Sudan na kuwa nchi huru mnamo 2011. Hata hivyo, kumekuwa na mzozo wa uongozi kati ya Rais Kiir na Naibu wake, Riek Machar.

Uhasama wa kisiasa umeiponza nchi hiyo pakubwa huku Machar akiunda jeshi la upinzani maarufu kama SPLA-IO.

Rais Museveni alionekana kuridhia ombi hilo lakini amesema suluhu ya kudumu ni kuandaliwa kwa uchaguzi wenye uwazi ambao hautaingiliwa na mrengo wowote wa kisiasa.

‘Kama kiongozi huwezi kushinda uchaguzi iwapo unaeneza chuki za kikabila kujitafutia umaarufu. Atapataje kura miongoni mwa makabila ambako anahubiri chuki na kuyagonganisha?’ amehoji Rais Museveni.

Rais wa Uganda ameishauri Sudan Kusini ianze kuwapa mazoezi ya kijeshi, wanajeshi wote kwa pamoja huku akisema hilo litasaidia kuzima makundi ya waasi yanayochipuka.

Tags