Mafuriko yaua 19 Sudan Kusini, malaki waachwa bila makazi
Mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa nchini Sudan Kusini yamesababisha vifo vya watu 19 na kuathiri wengine karibu 640,000 katika kaunti 26 katika majimbo sita ya nchi hiyo, hayo yamesemwa na Umoja wa Mataifa.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema katika taarifa yake ya jana Ijumaa kuwa, karibu watu 175,000 wameyahama makazi yao, na kujistri katika maeneo ya miinuko katika kaunti 16.
"Hatari za kiafya zinaongezeka, na kuongezeka kwa kesi za malaria, magonjwa ya kupumua, na kuharisha," OCHA imesema katika ripoti yake iliyotolewa huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini.
Imesema takriban vituo 121 vya afya vimeathiriwa huku kukiwa na ripoti 144 za watu kung'atwa na nyoka na visa 3,391 vya utapiamlo katika kaunti 11.
Ripoti hiyo imekuja siku moja baada ya shirika la misaada ya kimataifa la Save the Children kusema kuwa, takriban watu milioni 1.4 nchini Sudan Kusini wanakabiliwa na tishio la mafuriko mwaka huu, huku kukiwa na utabiri wa mvua nyingi katika mwezi huu wa Oktoba na Novemba.
Shirika hilo lilisema kuwa jamii tayari zimepoteza mashamba, makazi, na nyumba, huku wakishindwa kufikia shule na vituo vya afya. Inaarifiwa kuwa, watu 379,000 wamehama makazi yao kutokana na kuongezeka kwa maji ya mafuriko katika maeneo yao.
Save the Children pia imeripoti kuongezeka kwa magonjwa yanayosababishwa na maji machafu na kuongezeka kwa visa vya kung'atwa na nyoka, ambayo yanazidisha wasiwasi wa afya ya umma.