UN yalaani kuuawa askari wake wa kulinda amani Mali
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani mauaji ya askari watano wa kulinda amani wa Umoja huo nchini Mali ambao walipoteza maisha kufuatia hujuma ya kigaidi.
Katika taarifa, Baraza la Usalama limesisitiza kuhusu udharura wa kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria waliotekeleza hujuma hiyo ya kigaidi.
Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amelaani mashambulizi yaliyotokea nchini Mali na kusababisha vifo vya walinda amani watano kutoka Chad na kujeruhi wengine watatu.
Taarifa iliyotolewa na msemaji wake imeeleza kwamba msafara wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa (MINUSMA) ulilengwa kwa bomu lililotegwa ardhini kwenye eneo la Kidal kaskazini mwa nchi, na kisha ukashambuliwa na kundi la washambuliaji wasiojulikana.
Kundi la kigaidi linalojiita Ansaruddin tayari limetangaza kuhusika na shambulio hilo dhidi ya askari wa kimataifa wanaolinda amani kaskazini mwa Mali.
Askari wa kofia buluu wa Umoja wa Mataifa maarufu kwa jina la MINUSMA wako nchini Mali tangu mwaka 2013 kwa ajili ya kusaidia juhudi za kuleta utulivu katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Hata hivyo askari hao wamekuwa wakishambuliwa mara kwa mara na makundi yenye misimamo mikali katika maeneo hayo.