Amnesty International: Watoto wengi wanauawa au kusajiliwa na makundi ya kitakfiri
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuwa, watoto wengi wamekuwa wakisajiliwa na kutumiwa kama askari vitani na makundi ya kitakfiri au kuuawa na makundi hayo katika maeneo ya mpaka wa Burkina Faso, Niger na Mali
Ripoti iliyotolewa na Amnesty International inaeleza kuwa, makundi ya kitakfiri yanayoendesha harakati zao katika eneo la Sahel Afrika kila mwaka yamekuwa yakisajili wapiganaji wapya na inapotokea mtu kupinga kujiunga na makundi hayo basi huuawa.
Matthew Wells, Naibu Mkurugenzi wa Amnesty kitengo cha kukabiliana na mizozo amesema kuwa, makundi ya wanamgambo yamekuwa yakivamia shule mara kwa mara na yanawalenga watoto.
Matthe Wells anasema: Katika eneo la Tillaberi nchini Niger, kuna kizazi kinachokuwa ambacho kifo, woga na uharibifu vimetawala kkatika maisha yao.
Shirika hilo limeyalaumu makundi ya wanamgambo yenye mfungano na makundi ya kigaidi ya Daesh na al-Qaeda kwa masaibu yanayowakumba watoto katika eneo hilo.
Katika ripoti yake ya kurasa 63, Amnesty International inabainisha kwamba, watoto ndio wahanga wakuu wa harakati hizo za makundi ya kigaidi hasa katika mkoa wa Tillaberi wa Niger ambao unatajwa kuwa kitovu cha machafuko na harakati za makundi hayo ya kigaidi na kitakfiri.
Mashambulio ni sehemu ya machafuko makubwa yanayoshuhudiwa mara kwa mara katika mipaka ya Mali, Burkina Faso na Niger katika eneo la Sahel barani Afrika ambapo wapiganaji wa makundi ya waasi wanaohusishwa na al Qaeda na Daesh wanataka kulidhibiti eneo hilo.