Algeria yakadhibisha madai ya Morocco kuhusu kuwepo Hizbullah huko Tindouf
Algeria imekadhibisha madai yaliyotolewa na Morocco kwamba wapiganaji wa harakati ya Hizbullah wako katika mji wa Tindouf kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wapigania uhuru wa Polisario huko Sahara Magharibi. Algeria imeyataja madai hayo kuwa ni uongo mtupu.
Jarida la al Jeishi linalomilikiwa na Jeshi la Algeria limetangaza kuwa, matamshi yaliyotolewa na mwakilishi na balozi wa Morocco katika Umoja wa Mataifa, Omar Hilale, kuhusu kuwepo watu wenye mfungamano ya Hizbullah ya Lebanon katika mji wa Tindouf ulioko kwenye mpaka wa Algeria na Sahara Magharibi kwa shabaha ya kutoa mafunzo kwa wapiganaji wa Polisario ni uongo unaomstaajabisha kila mtu. Jarida hilo limeongeza kuwa, Omar Hilale anataka kuwaambia Wazayuni wa Israel kwamba, adui wao yaani Hizhullah ya Lebanon yuko nchini Algeria na ni hatari kwa rafiki wenu yaani Morocco. Matamshi hayo ya Balozi wa Morocco katika UN pia yanatoa ujumbe kwa nchi za Magharibi kwamba Hizbullah ni kundi la kigaidi na kwamba wapiganaji wake wamepelekwa katika ardhi ya Algeria huko Tindouf kwa ajili ya kuvuruga amain na kuishambulia Morocco.
Madai hayo ya Morocco yametolewa baada ya Algeria kuituhumu nchi hiyo na sahiba wake, Israel, kuwa zimehusika katika moto ulioteketeza misitu ya Algeria na kuua makumi ya watu.
Tarehe 24 Agosti Algeria ilichukua hatua ya kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Morocco ikiituhumu Rabat kuwa imehusika na hatua kadhaa za kiuadui na kiuhasama dhidi yake.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Algeria Ramtane Lamamra amesema uamuzi huu hauwezi kubadilika, umechukuliwa kwa kuzingatia maslahi ya taifa na kwamba, Algeria imekuwa na subira muda mrefu kabla ya kuchukua uamuzi huo ikivumilia chokochoko za jirani yake Morocco.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, Morocco ilikubali kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel kwa sharti kwamba, Marekani iafiki mpango wa kuliunganisha eneo la Sahara Magharibi na ardhi ya nchi hiyo. Baada ya hapo rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuwa Sahara Magharibi ni sehemu ya ardhi ya Morocco. Hata hivyo kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Uadilifu ya Ulaya, hadi sasa nchi nyingi zimekataa kuitambua Sahara Magharibi kuwa ni sehemu ya ardhi ya Morocco.