Wanafunzi 26 waaga dunia katika mkasa wa moto shuleni Niger
(last modified Tue, 09 Nov 2021 03:23:40 GMT )
Nov 09, 2021 03:23 UTC
  • Wanafunzi 26 waaga dunia katika mkasa wa moto shuleni Niger

Wanafunzi wasiopungua 26 wameaga dunia katika mkasa wa moto ulioikumba shule moja nchini Niger.

Shirika la habari la AFP limenukuu vyanzo vya habari vikisema kuwa, ajali hiyo ya moto imetokea usiku wa kuamkia leo katika shule moja iliyoko katika jimbo la Maradi, kusini mwa nchi.

Chaibou Aboubacar, meya wa jiji la Maradi amesema kufikia sasa wanafunzi 26 wamethibitishwa kuaga dunia katika mkasa huo, huku wengine 13 wakijeruhiwa. 

Inaarifiwa kuwa, moto huo ulienea kwa kasi kwa kuwa madarasa ya shule hiyo ya msingi yamejengwa kwa mbao na mapaa ya majani makavui. Siku tatu za kuomboleza mkasa huo imetangazwa katika jimbo la Maradi. 

Haya janajiri muda mfupi baada ya wachimba migodi 18 kufariki dunia baada ya kuporomokewa na udongo kwenye mgodi wa dhahabu kusini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, mpakani na Nigeria.

Wachimba migodi kazini

Adamou Gueraou, meya wa wilaya ya Dan-Issa amesema wachimba migodi hao walioaga dunia walizikwa jana Jumatatu, na kwamba majeruhi saba wa mkasa huo wamelazwa hospitalini. Habari zaidi zinasema kuwa, ajali hiyo ilitokea juzi Jumapili katika timbo la Garin-Liman, linalopatikana katika jimbo la Maradi, kusini mwa nchi.

Takwimu zinaonyesha, aghalabu ya madini hususan ya dhahabu yanayochimbwa kinyume cha sheria nchini Niger pamoja na nchi nyingine za Afrika, husafirishwa kimagendo katika nchi za Ulaya na Uarabuni.  

Tags