25 wauawa katika shambulio la wabeba silaha Niger
(last modified Thu, 18 Nov 2021 02:57:03 GMT )
Nov 18, 2021 02:57 UTC
  • 25 wauawa katika shambulio la wabeba silaha Niger

Watu wasiopungua 25 wameuawa katika shambulio la watu waliobeba silaha huko kusini magharibi mwa Niger.

Attawane Abeitane, meya wa mji wa Tillia alinukuliwa jana Jumatano na shirika la habari la Reuters akisema kuwa, wabeba silaha hao waliokuwa wamepanda pikipiki walishambulia kambi ya askari jamii karibu na kijiji cha Bakorat katika eneo Tahou na kufanya umwagaji damu huo.

Amesema wabeba silaha hao wanaonekana kutoka maeneo ya mbali na kuvamia vijiji vyao, na kwamba kadhaa miongoni mwao wameuawa, huku pikipiki zao zikichomwa moto.

Hakuna genge lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo, lakini inaaminika kufanywa na moja kati ya makundi yanayobeba silaha yenye mfungamano na makundi ya kigaidi ya Daesh (ISIS) na al-Qaeda, ambayo yanaendesha operesheni zao katika eneo la Sahel, magharibi mwa Afrika.

Ramani ya Niger inayoonesha eneo la Tillaberi linaloaminika kuwa ngome ya wabeba silaha

Mapema mwezi huu, shambulio jingine la genge la wabeba silaha liliua watu karibu 70 wasio na hatia katika eneo la Tillabery, kusini magharibi mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, makundi yanayobeba silaha yameua watu karibu 600 katika maeneo ya kusini magharibi mwa Niger.

Tags