Umoja wa Mataifa watoa wito wa kuhitimishwa vita kaskazini mwa Ethiopia
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuhitimishwa vita na mapigano kati ya serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) kaskazinii mwa nchi hiyo.
Antonio Guterres amesema kuwa, umoja huo unazitaka pande mbili kukomesha vita na kuanza kufanya mazungumzo jumuishi kwa shabaha ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa takwa hilo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Abiy Ahmed Waziri Mkuu wa Ethiopia na Debretsion Gebremichael, kiongozi wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF).
Guterres amezitaka pande hizo mbili kuhitimisha vita na hivyo kuandaa uwanja wa kufanyika mazungumzo jumuishi ili kuzipatia ufumbuzi hitilafu zilizo baina ya pande mbilii.
Wakati huo huo msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema kuwa, madereva wote Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) waliokamatwa wiki moja iliyopita nchini Ethiopia wameachiliwa huru.
Takriban madereva 70 walikamatwa kwenye mji mkuu wa jimbo la Afar ambao uko kwenye barabara pekee iliyobaki ya kupeleka misaada kwenye eneo lililokumbwa na mzozo la kaskazini la Tigray.
Madereva hao walikamatwa baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kutangaza hali ya dharura mapema mwezi huu baada ya vikosi vya TPLF kudai kwamba, vilikuwa vikielekea kwenye mji mkuu Addis Ababa.
Mapigano yanayojiri huko Tigray hadi sasa yamesababisha watu karibu milioni mbili kuwa wakimbizi na wengine laki nne kukabiliwa na ukosefu wa chakula.