Niger kununua silaha na zana za kijeshi kutoka Uturuki
(last modified Sun, 21 Nov 2021 03:02:20 GMT )
Nov 21, 2021 03:02 UTC
  • Niger kununua silaha na zana za kijeshi kutoka Uturuki

Niger na Uturuki zimetangaza kufikia makubaliano ambayo yanajumuisha kuiuzia Niger silaha mbalimbali zikiwemo ndege zisizo na rubani (droni) na magari ya kivita ili kuongeza uwezo wake wa kijeshi katika kukabiliana na makundi ya kigaidi.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na televisheni ya Uturuki ya TRT na Ofisi ya Rais wa Niger imeeleza kuwa: "Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ametangaza katika mazungumzo yake ya simu na Rais wa Niger, Mohamed Bazoum kwamba, droni aina ya TP2, ndege ya mafunzo aina ya Hurkosh na magari ya deraya ambayo Niger itanunua kutoka Uturuki yataimarisha uwezo wa jeshi na vikosi vyake vya ulinzi." 

Rais Erdogan wa Uturuki afanya mazungumzo ya simu na Rais Bazoum wa Niger 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Rais Erdogan aidha ametoa mkono wa pole na taazia kwa wahanga wa mashambulizi ya Jumanne iliyopita huko magharibi mwa Niger na kusisitiza kuwa Uturuki inaunga mkono juhudi za Niamey za kupambana na ugaidi." 

Inafaa kuashiria hapa kuwa, makampuni ya Kituruki yanapanua uwepo wake huko Niger ambako hadi sasa yamefanikiwa kufunga mikataba kadhaa ikiwa ni pamoja na mkataba wa yuro milioni 152 wa kukarabati uwanja wa ndege wa Niamey, mkataba wa yuro milioni 50 wa kujenga hoteli ya kifahari na ule wa thamani ya yuro milioni 38 wa kujenga makao makuu mapya ya Wizara ya Fedha huko Niger. 

Tags