Ripoti: Misri ilitumia taarifa za kijasusi za Ufaransa kuua raia
(last modified Mon, 22 Nov 2021 12:03:36 GMT )
Nov 22, 2021 12:03 UTC
  • Ripoti: Misri ilitumia taarifa za kijasusi za Ufaransa kuua raia

Ripoti mpya imefichua kuwa, vikosi vya usalama vya Misri vimetumia taarifa za kiintelijensia za jeshi la Ufaransa kuwahujumu na hata kuwaua raia wa nchi hiyo ya Kiarabu wanaotuhumiwa kufanya magendo.

Ripoti ya uchunguzi uliofanywa na taasisi ya 'Disclose' kwa kutegemea nyaraka zilizovuja imeeleza kuwa, jeshi la Ufaransa lilihusika na angalau mashambulio 9 ya anga yaliyofanywa na jeshi la Misri dhidi ya raia baina ya mwaka 2016 na 2018.

Inaelezwa kuwa, Ufaransa na Misri zilifanya hujuma hizo katika operesheni iliyopewa jina la Operesheni ya Sirli, iliyolenga zaidi maeneo ya mpaka wa magharibi wa Misri na Libya.

Ripoti hiyo ya Disclose imebainisha kuwa, awali operesheni hiyo ilikuwasudiwa kuwa ya kupambana na magenge ya kigaidi, lakini iliishia kuwa hujuma dhidi ya raia wa nchi hiyo ya Kiarabu kwa msaada wa ujasusi wa Ufaransa.

Rais Sisi wa Misri

Tangu operesheni hiyo ianze Februari mwaka 2016 wakati wa utawala wa aliyekuwa rais wa Ufaransa, Francois Hollande, serikali ya Paris imeiuzia Misri silaha na zana za kijeshi zenye thamani na mabilioni ya dola.

Katika miezi ya karibuni, asasi nyingi za kimataifa na za kutetea haki za binadamu zimetoa indhari kuhusu utendaji wa utawala wa Misri unaoongozwa na Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri katika masuala ya uhuru wa kijamii na kisiasa na ukiukaji wa haki za binadamu.

 

 

Tags