Ufaransa yamkamata mwanaharakati anayepinga ukoloni Afrika
(last modified 2024-10-16T07:09:22+00:00 )
Oct 16, 2024 07:09 UTC
  • Ufaransa yamkamata mwanaharakati anayepinga ukoloni Afrika

Mwanaharakati na mwanamajimui mashuhuri wa kupinga ukoloni mamboleo barani Afrika, Stellio Gilles Robert Capo Chichi, maarufu kama Kemi Seba, amekamatwa nchini Ufaransa.

Shirika la habari la Anadolu limeandika habari hiyo na kueleza kuwa, duru za mahakama jana Jumanne zilithibitisha kuwa, Seba ambaye amewahi kuhukumiwa mara kadhaa nchini Ufaransa kwa madai ya kuchochea ubaguzi wa rangi, ametiwa mbaroni.

Mwanaharakati huyo mwenye uraia pacha wa Ufaransa na Benin, na ambaye pia ni Rais wa shirika lisilo la kiserikali la Urgences Panafricanistes, alikamatwa Jumatatu mjini Paris pamoja na Hery Djehuty, mratibu wa shirika hilo.

Katika miaka ya karibuni, Seba , 42, ameandaa au kushiriki maandamano kadhaa dhidi ya Jumuiya ya Kifedha ya Afrika (CFA franc), ambapo amekuwa akikamatwa na kufukuzwa Ufaransa mara kwa mara.

Mwanahakati huyo ambaye ni mzawa wa Ufaransa na wazazi kutoka Benin, anajulikana sana kwa msimamo wake dhidi ya Magharibi na ukuruba wake na Moscow.

Sababu ya kukamatwa kwake bado haijawekwa wazi. Mnamo Julai mwaka huu, mamlaka za Ufaransa zilibatilisha uraia wake.

Seba ni mwanaharakati mwenye ushawishi mkubwa katika duru za Waafrika, ambapo amekuwa akifanya kampeni kubwa ya kupigania ukombozi na uhuru kamili wa Afrika kutoka kwenye minyororo ya wakoloni.

Tags