Madaktari Angola kuendelea na mgomo wa nchi nzima
(last modified Mon, 13 Dec 2021 04:31:12 GMT )
Dec 13, 2021 04:31 UTC
  • Madaktari Angola kuendelea na mgomo wa nchi nzima

Zaidi ya nusu ya madaktari wote nchini Angola wanaendelea na mgomo wao wa nchi nzima wakishinikiza kulipwa mishahara yao na kuboreshewa mazingira ya kazi huku janga la corona likiendelea kuutatiza mfumo dhaifu wa huduma za afya wa nchi hiyo.

Mwaka jana serikali ya Angola iliomba msaada kutoka China na Cuba ili kuweza kukabiliana na janga la Covid-19 ambapo madaktari wa Cuba zaidi ya 250 waliwasili nchini humo. Takwimu za mwaka jana zinaonyesha kuwa Angola ina jumla ya madaktari 5,200. 

Muungano wa Taifa wa Madaktari wa Angola umesema kuwa wanachama wake 3000 wataendelea kufanya mgomo wa kitaifa katika vituo vyote vya umma baada ya kuanza mgomo wao wiki iliyopita. Madaktari hao wanadai nyongeza ya mishahara na mafao mengine wakati wa kazi za dharura. 

Muungano wa Madaktari wa Angola umeongeza kuwa, wagonjwa mahututi pekee ndio watakaohudumiwa katika kitengo cha huduma za dharura wakati mgomo wa kitaifa ukiendelea nchi nzima, na madaktari waliosalia kazini ni nusu ya idadi kamili. Muungano huo umeipatia serikali ya Rais Joao Lourenco muhula wa siku 30 ili kushughulikia matakwa yao huku mazungumzo yakiendelea.  

Wagonjwa mahututi wakipatiwa huduma katika kitengo cha dharura 

Angola, nchi tajiri kwa madini mbalimbali na kubwa ya katikati mwa bara la Afrika ambayo ina watu milioni 33, inataabika na umaskini licha ya kuwa na utajiri wa mafuta.  Watu wasiopungua 65,400 wameambukizwa ugonjwa wa corona nchini Angola hadi sasa na wengine zaidi ya 1,700 wameaga dunia kwa maradhi hayo.