Algeria yasisitizia ulazima wa kuweko umoja wa Wapalestina
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Algeria amesisitiza udharura wa kuweko umoja na mshikamano baina ya Wapalestina.
Ramtane Lamamra amesema kuwa, katika kikao cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Kiarabu kilichoitishwa hivi kariibuni kulijadiliwa matukio katika mataifa ya Kiarabu na masuala mengine yanayohusiana na kutoa himaya na kuimarisha ushirikiano wa pamoja baina ya mataifa hayo kieneo na kimataifa katika kipindi cha baada ya janga la Corona.
Wakati huo huo ujumbe wa Harakati ya Wananchi Kwa Ajili ya Ukombozi wa Palestina umetangaza kuwa, Algeria inataka kuweko mafanikio katika mikutano na mazungumzo ya Wapalestina.
Siku chache zilizopita pia, Rais wa Algeria alitangaza pia kuwa nchi yake itaendelea kulitetea taifa la Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.
Rais Abdelmadjid Tebboune alisisitiza kuwa, kuitetea Palestina ni katika vipaumbele vya serikali yake na kuongeza kuwa, hakuna upande wowote wa kigeni unaoweza kubadili msimamo huo wa Algeria.
Katika miezi ya hivi karibuni nchi ya Algeria imekuwa mstari wa mbele kupinga sera na siasa za utawala ghasibu wa Israel na ukandaizaji wake dhidi ya wananchi wa Palestina.
Misimamo hiyo ya Algeria imeshuhudiwa zaidi baada ya jirani yake, Morocco, kutia saini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na kutia saini hati ya kuanzisha ushirikiano wa kijeshi na utawala huo ghasibu.