AU yatiwa wasi wasi na jaribio la mapinduzi Guinea-Bissau
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i79918-au_yatiwa_wasi_wasi_na_jaribio_la_mapinduzi_guinea_bissau
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat amesema AU imesikitishwa mno na jaribio la mapinduzi lililofeli katika nchi nyingine ya Afrika Magharibi ya Guinea-Bissau.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 03, 2022 02:31 UTC
  • Moussa Faki Mahamat
    Moussa Faki Mahamat

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat amesema AU imesikitishwa mno na jaribio la mapinduzi lililofeli katika nchi nyingine ya Afrika Magharibi ya Guinea-Bissau.

Taarifa ya AU inasema: Mwenyekiti Mahamat amelitaka jeshi kurejea kambini haraka iwezekanavyo, kuwadhaminia usalama Rais Umaro Sissoco Embalo wa nchi hiyo pamoja na maafisa wengine wa serikali, na kuwaachia huru kadhaa waliokamatwa miongoni mwao.

Kabla ya hapo, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS ililaani jaribio hilo la mapinduzi huko Guinea-Bissau na kulitaka jeshi la nchi hiyo kurejea katika kambi zake.

Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema ametiwa hofu kubwa na hali ya mambo huko Guinea-Bissau baada ya kuzimwa jaribio hilo la mapinduzi dhidi ya serikali ya Rais Embalo. 

Rais Umaro Sissoco Embalo wa Guinea-Bissau

Jaribio la mapinduzi lililofeli liliripotiwa kutokea juzi Jumanne huko Guinea-Bissau baada ya watu kadhaa wasiojulikana waliokuwa wamevaa mavazi ya kiraia kuanza kufyatua risasi karibu na jengo la serikali ambako Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri wa serikali walikuwa na mkutano. 

Rais Umaro Sissoco Embalo wa Guinea-Bissau amesema kuwa jaribio la mapinduzi lililokusudiwa kumuondoa madarakani limefeli na amewatolea wito wananchi kote nchini kuwa watulivu.