Jumapili, 25 Mei, 2025
Leo ni Jumapili 27 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1446 Hijria, mwafaka na 25 Mei 2025 Miladia.
Trehe 4 Khordad kwa mujibu wa kalenda ya Iran ya Hijria Shamsia imepewa jina la Siku ya Kusimama Kidete Dezful, ambao ni moja ya miji ya kusini mwa Iran. Sababu ya siku hii kupewa jina hilo ni muqawama na ungangari wa watu wa Dezful kukabiliana na hujuma na mashambulio ya makombora ya utawala wa Kibaathi wa Iraq wakati wa vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Wakati vilipoanza vita hivyo vya Kujihami Kutakatifu, mji wa Dezful ulishambuliwa kwa makombora zaidi ya 200 na kwa risasi zaidi ya elfu ishirini mpaka ukajulikana kwa jina la mji wa makombora. Pamoja na yote hayo wananchi katika mji wa Dezful waliendelea kuonyesha muqawama na uhimilivu kiasi kwamba hata katika mazingira hayo Sala ya Ijumaa iliendelea kusaliwa kila wiki kwa kuhudhuriwa na wananchi na wapiganaji waliokuwa kwenye medani za vita.

Miaka 104 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibuu wa kalenda ya Hijria Shamsia, Sayyid Ziauddin Tabatabai aliondolewa katika wadhifa wa Waziri Mkuu kwa amri ya Ahmad Shah Qajar. Ziauddin alishiriki katika mapinduzi ya Rizakhan ya 1299 Hijria shamsia kwa himaya ya Uingereza. Katika siku za kwanza za kuwasili kwa vikosi vya Kazakh huko Tehran, Seyyed Ziauddin alikutana na Ahmad Shah na akapokea agizo la kuwa Waziri Mkuu akiwa na mamlaka kamili. Katika siku ya kwanza ya uongozi wake, alichukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwakamata takriban viongozi mia mbili wa nchi hiyo na wanazuoni. Hatua ya kuporomoka kwa serikali ya Seyyed Ziauddin Tabatabai, inayojulikana kama Serikali ya nyeusi na Baraza la Mawaziri la Siku Mia, inapaswa kutambuliwa katika kutofautiana kwake na kamanda mkuuu wa majeshi.

Siku kama ya leo, miaka 665 iliyopita, yaani tarehe 25 Mei mwaka 1360 kundi la mabaharia wa Kifraransa liligundua Ghuba ya Guinea. Ghuba ya Guinea iko magharaibi mwa bara la Afrika katika bahari ya Atlantiki. Baada ya muda kupita tangu kugunduliwa Ghuba ya Guinea, ushawishi wa Ufaransa ndani ya bara hilo ulianza, na taratibu ikaanza kuidhibiti ardhi iliyokuja kujulikana baadaye kama Guinea. Nchi ya Guinea iliendesha harakati za mapambano ya miaka mingi mpaka ikafanikiwa kupata uhuru wake mwaka 1958. Guinea ina eneo lenye ukubwa wa kilomitamraba zaidi 245,000 na imepakana na nchi za Senegal, Guinea Bissau, Mali, Ivory Coast, Liberia na Sierra Leone. ***

Miaka 62 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 25 Mei mwaka 1963, Hati ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) ilisainiwa mjini Addis Ababa, Ethiopia kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi 32 za bara hilo. Marais Gamal Abdel Nasser wa Misri, Kwame Nkrumah wa Ghana na Ahmed Sekou Toure wa Guinea walikuwa miongoni mwa waasisi wa jumuiya hiyo. Jumuiya ya OAU ilielekeza jitihada zake katika kuleta umoja kati ya nchi za Afrika, kutatua hitilafu kati ya nchi hizo, kutetea haki ya kujitawala ya nchi wanachama na ukombozi wa nchi nyingine za Kiafrika zilizokuwa zingali zinakoloniwa. Mnamo mwezi Julai mwaka 2002, viongozi wa nchi wanachama wa OAU walifanya kikao nchini Afrika Kusini na kuamua kubadilisha jina la jumuiya hiyo kutoka Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) na kuwa Umoja wa Afrika (AU) sambamba na kuanzisha taasisi kadhaa kwa ajili ya utekelezaji wa maamuzi ya umoja huo na kustawisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama. Hivi sasa Umoja wa Afrika una nchi 54 wanachama. Makao Makuu ya umoja huo yako Addis Ababa, Ethiopia na kikao cha viongozi wa nchi wanachama hufanyika kila mwaka katika moja ya nchi hizo. ***

Miaka 10 iliyopita katika siku kama ya leo yaani 27 Dhulqaada mwaka 1436 Hijria Qamaria winchi kubwa ya ujenzi ilianguka katika eneo moja la Msikiti Mtakatifu wa Makka na kuua idadi kubwa ya mahujaji wa Baitullah al-Haram yaani Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu. Tukio hilo lilijiri Ijumaa saa 17:10 alasiri Septemba 11 mwaka 2015 ambapo winchi hiyo ilipelekea watu 107 kupoteza maisha na wengine 238 kujeruhiwa. Aghalabu ya waliopoteza maisha walikuwa ni mahujaji kutoka nchi za India, Pakistan, Indonesia na Iran. Wakuu wa Saudia walisema winchi hiyo ilianguka kutokana na upepo mkali. Tukio hilo la kusikitisha lilionyesha uzembe wa hali ya juu wa utawala wa Saudia. Tukio hilo la kuanguka winchi na maafa ya Mina wakati wa Sikukuu ya Idul Adha mwaka huo huo ni kati ya matukio machungu zaidi yaliyoshuhudiwa katika ibada ya Hija. ***
