Malawi kutokuwa na umeme kwa muda wa miezi sita kufuatia kimbunga kikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i80122-malawi_kutokuwa_na_umeme_kwa_muda_wa_miezi_sita_kufuatia_kimbunga_kikali
Kituo kikuu cha kusambaza nishati ya umeme nchini Malawi hakifanyi kazi baada ya bwawa la Chikwawa kuathiriwa pakubwa na mvua nkali zilizosababishwa na kimbunga kikubwa cha kitropiki cha Ana tarehe 24 mwezi Januari mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 08, 2022 12:03 UTC
  • Malawi kutokuwa na umeme kwa muda wa miezi sita kufuatia kimbunga kikali

Kituo kikuu cha kusambaza nishati ya umeme nchini Malawi hakifanyi kazi baada ya bwawa la Chikwawa kuathiriwa pakubwa na mvua nkali zilizosababishwa na kimbunga kikubwa cha kitropiki cha Ana tarehe 24 mwezi Januari mwaka huu.

Kampuni ya Taifa ya Umeme ya Malawi (EGENCO) imetangaza kuwa nchi hiyo inatazamia kubakia bila ya umeme kwa muda wa miezi sita. Watu zaidi ya 90 wamepoteza maisha kufuatia kimbunga hicho kilichoziathiri nchi za kusini mwa Afrika. 

Mkurugenzi wa Kampuni ya Taifa ya Umeme ya Malawi, Willy Liabunya ameeleza kuwa, madhara yaliyosababishwa na kimbunga cha Ana nchini humo ni pamoja na kuharibiwa bwawa linalohusika na uzalishaji wa umeme.  Amesema, maeneo mengi ya Malawi hayana umeme hivi sasa kutokana na mvua kubwa zilizonyesha na kuathiri vituo vya kuzalisha nishati hiyo. 

Kimbunga cha Ana kilichoziathiri nchi za kusini mwa Afrika ikiwemo Malawi 

Mkurugenzi huyo wa EGENCO ameongeza kuwa, kampuni hiyo inajipanga kwa ajili ya kupata utatuzi wa muda wa kurejesha haraka mitambo ya kuzalisha umeme na kwamba wanadhani kuwa muda wa miezi sita utatosha kushughulikia suala hilo. 

Hadi sasa maafisa husika wa Malawi wamethibitisha kuwa zaidi ya watu 100 wamejeruhiwa vibaya katika wilaya 15 baada ya mvua kunyesha kwa zaidi ya wiki moja. Idara ya Kushughulikia Majanga na Maafa ya Kimaumbile ya Malawi imeripoti kuwa, watu zaidi ya laki mbli kutoka familia elfu 48 wameathiriwa na mvua kubwa na kulazimika kuhama makazi yao.